HabariHabari za KauntiHabari za Kitaifa

Gavana akana dai hofu ya uchawi ilimfukuza ofisini

Na WINNIE ATIENO November 3rd, 2026 Kusoma ni dakika: 1

GAVANA wa Tana River, Bw Dhadho Godhana, ameeleza sababu zinazomfanya kutotumia mara kwa mara ofisi yake rasmi mjini Hola, na badala yake kufanyia kazi katika maeneo mengine, yakiwemo afisi za mahusiano ya nje ya kaunti yake zilizo mjini Mombasa na Nairobi.

Bw Godhana alipuuzilia mbali madai kwamba hofu ya uchawi ndiyo iliyomlazimu kuachana na ofisi yake ya Hola, akifafanua kuwa kufanya kazi kutoka maeneo mengine ni mkakati wa kudhibiti umati wa watu na kuhakikisha usalama.

Alisema amekuwa akipunguza kwa makusudi ziara zake katika jengo kuu la utawala wa kaunti kutokana na uhaba mkubwa wa nafasi na uwezekano wa wananchi kusababisha vurugu.

Akizungumzia uvumi ulioibuka kufuatia tukio la mwaka wa 2019 ambapo paka aliyechinjwa alipatikana katika majengo ya Bunge la Kaunti ya Tana River, Bw Godhana alikiri kuwa uchawi ni imani inayoshikiliwa na baadhi ya watu katika jamii, lakini akasisitiza kuwa hauhusiani kwa vyovyote na maamuzi yake kuhusu maeneo anayofanyia kazi.

Katika mahojiano na kituo cha runinga cha NTV, alibainisha kuwa hufanyia kazi katika maeneo mbalimbali, yakiwemo makazi yake binafsi.

Hata hivyo, aliongeza kuwa serikali ya kaunti inaendelea kujenga jengo la kisasa la utawala litakalowezesha shughuli zote za serikali ya kaunti kuendeshwa katika eneo moja.