Habari

Majonzi watu sita wakifariki baada ya gari lao kutumbukia mtoni

Na MWANGI MUIRURI October 26th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

MUME, mke na mwana wao wa kiume walikuwa kati ya watu sita ambao waliaga dunia Jumamosi usiku wakati ambapo gari walilokuwa wakisafiria lilitumbukia ndani ya mto katika Kaunti ya Murang’a.

Kwa mujibu wa polisi, ajali hiyo ilisababisha ndugu watatu kupoteza maisha yao pamoja na mke wa mmoja wao, mwana wa wanandoa hao na mwanamke ambaye bado hajatambuliwa.

Kamanda wa Kaunti ya Murang’a, Charles Muriithi, alisema sita hao walikuwa wametoka hafla ya ulipaji mahari Kaunti ya Kiambu. Waliangamia wakati ambapo matatu yao yenye uwezo wa kuwabeba abiria 14 ilitumbukia Mto Kiama, eneobunge la Gatanga.

“Ajali hiyo ilifanyika katika Barabara ya Chomo-Kahunyu. Waliojeruhiwa walipelekwa katika Hospitali ya Kirwara Level Four na Hospitali ya Murang’a Level Five. Tunathibitisha kuwa sita kati yao wamefariki,” akasema Bw Muriithi.

Ripoti ya polisi kuhusu ajali hiyo ilithibitisha kuwa walioaga dunia ni Amos Kihara Kamau, Alice Wambui Mwangi, Elijah Kamau Macharia, Peter Mwangi Macharia, Paul Karanja Macharia na mwanamke ambaye jina lake halikuwa limetambuliwa.

“Mwanamke huyo hakuwa na kitambulisho na alikuwa ameabiri gari hilo njiani. Ni dereva ambaye sasa ameaga ndiye huenda alimjua,” akasema Bw Mbatia.

“Nilikuwa hata nimewasaidia kwenye safari ya kulipa mahari katika kijiji cha Nazereth, Kaunti ya Kiambu na habari kuhusu mauti yao ilinisikitisha sana,” akasema.

Afisa wa Afya wa Kaunti ya Murang’a, Eliud Maina, alisema gari hilo lilikuwa na watu 16 na mtoto mmoja.

“Sita waliletwa Hospitali ya Murang’a Level Five wakiwa tayari wameaga dunia na baada ya hilo kuthibitishwa na madaktari wetu, tuliwapeleka hadi makafani,” akasema.

Bw Maina aliongeza kuwa wengine wawili wapo katika hali mbaya kiafya, wawili wakiwa na majera makubwa huku wengine wakiwa na majeraha madogo.

“Ajali hiyo iliishia kuwa mbaya zaidi kutokana na giza ambalo lilikuwa limetanda. Majeruhi wengine walikuwa wakihepa kuondoka mtoni huku wengine wakiwa ndani ya magari yao.”