Habari

Majuto ya ufisadi

June 26th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

RICHARD MUNGUTI na BENSON MATHEKA

HUKUMU kali aliyopewa Mbunge wa Sirisia John Waluke na mshtakiwa mwenzake Grace Wakhungu mnamo Alhamisi ya kulipa jumla ya Sh2.1 bilioni, ama kifungo cha miaka saba gerezani, imezua hofu miongoni mwa washukiwa wengine wanaokabiliwa na kesi za ufisadi hasa wanasiasa.

Hii ni kutokana na kuwa adhabu hiyo ya kihistoria huenda ikatumika kama kigezo katika kuamua kesi zingine za ufisadi.

Bw Waluke na Bi Wakhungu walipatikana na makosa ya wizi wa Sh313 milioni kwa kupokea pesa hizo kwa njia haramu kutoka kwa Bodi ya Nafaka (NCPB) mnamo 2014.

Hakimu Mkuu Grace Juma aliagiza wawili hao kulipa faini pamoja na pesa zingine kwa NCPB, akisema walipokea pesa hizo licha ya kuwa hawakuuza mahindi yoyote.

Mara baada ya hukumu, wawili hao walipelekwa gerezani kuanza kifungo baada ya Bi Juma kukataa ombi la mawakili wao kuwa aahirishe kuanza kwa kifungo.

Mawakili hao wanatarajiwa kukata rufaa dhidi ya hukumu hiyo ambayo ni ya kihistoria nchini.

Hukumu hiyo ni ushindi mkubwa kwa Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) ambaye amekuwa akilaumiwa kwa kukosa kuendesha kesi za ufisadi kwa njia ambayo washukiwa wameweza kupatikana na makosa na kuhukumiwa.

Pia inatoa msingi wa mahakimu na majaji kutoa adhabu kali kwa wanaopatikana na makosa ya ufisadi, kwani awali wengi wamekuwa wakitozwa faini ya chini sana ikilinganishwa na kiasi cha pesa walizoiba.

Hii ndiyo sababu hukumu hiyo imezua wasiwasi miongoni mwa washukiwa wa ufisadi kwani imeweka msingi wa mahakimu na majaji kuendeleza msururu wa adhabu kali, bila kujali vyeo vyao wahusika katika jamii.

Kati ya wanasiasa ambao wana kila sababu ya kuwa na wasiwasi ni aliyekuwa Gavana wa Nairobi Evans Kidero, ambaye ana kesi mbili za ufisadi za mamilioni ya pesa katika mahakama ya ufisadi.

Kesi ya kwanza dhidi ya Bw Kidero inahusu malipo ya Sh68 milioni kwa kampuni ya mawakili kinyume cha sheria alipokuwa gavana na nyingine inayohusu wizi wa Sh213 milioni.

Gavana wa Nairobi Mike Sonko naye ameshtakiwa kwa madai ya kuhusika katika wizi wa Sh357milioni za serikali ya kaunti yake.

Aliyekuwa gavana wa Kiambu Ferdinard Waititu na mkewe nao wanakabiliwa na kesi ya wizi wa Sh588 milioni za kaunti hiyo huku Gavana wa Samburu Moses Kasaine akiwa na kesi ya wizi wa Sh84 milioni za kaunti yake.

Mbunge wa Lugari Ayub Savula naye ana kesi ya kupora Sh122 milioni kutoka kwa shirika la matangazo la serikali.

Wengine walio na kesi ni aliyekuwa waziri wa fedha Henry Rotich, na aliyekuwa waziri wa michezo Hassan Wario miongoni mwa wengine.

Bw Waluke alipatikana na hatia ya kupokea pesa hizo katika kashfa ya mahindi ya mwaka wa 2014.

Upande wa mashtaka ulithibitisha kuwa washtakiwa walipokea pesa kwa njia ya undanganyifu kupitia kwa kampuni yao Erad Supplies and General Contractors Limited.