Makachero wa EACC wavamia makazi ya Gavana
MAKAZI ya Gavana wa Nyamira Amos Nyaribo jana yalivamiwa na Makachero wa Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi Nchini (EACC) kuhusiana na wizi wa mamilioni ya fedha za umma.
Makachero walivamia na kupekua makazi ya Bw Nyaribo mtaani Karen Nairobi pamoja na nyumba zake kaunti za Kisii na Nyamira.
Pia makachero hao walilenga maafisa wa ngazi ya juu katika serikali ya kaunti hiyo. Maafisa hao wanashukiwa kupanga njama na kushirikiana na Bw Nyaribo kutoa malipo kwa kaunti bila kufuata kanuni zinazohitajika kisheria.
Kwa mujibu wa EACC, walivamia makazi ya gavana kuhusiana na kandarasi ya Sh382 milioni ambayo ilikuwa ya ujenzi wa afisi za serikali ya Kaunti ya Nyamira.
Tenda hiyo ilitolewa kwa kampuni ya Uhandisi ya Spentch na ilidaiwa ilikuwa na malipo ambayo hayakutolewa kwa njia inayostahili.
Wachunguzi wanaamini kampuni hiyo ilipokea malipo ambayo yalikuwa ya kiwango cha juu ikilinganishwa na kazi ambayo ilikamilishwa.
Ripoti ya awali inaonyesha hasara ambayo ilipatikana na serikali ya kaunti na haikuwiana na thamani ya pesa ambazo zilitumika.
EACC ilisema lengo la uvamizi huo lilikuwa kupata stakabadhi muhimu na ushahidi ambao utachangia kufahamu jinsi ambavyo kandarasi hiyo ilitolewa.
“Wachunguzi wetu wanasaka maelezo ya kuonyesha pesa hizo zilifujwa kutokana na bei ya vifaa vilivyotumika kuongezwa,” akasema Afisa wa ngazi ya juu wa EACC ambaye hakutaka jina lake linukuliwe.
Kando na zabuni ya Sh382 milioni, EACC pia inachunguza madai kuwa Gavana Nyaribo bila kufuata sheria, alijilipa jumla ya Sh5 milioni na pia Sh3 milioni nyingine kama marupurupu ya nyumba.
Maafisa wengine wa kaunti ambao wanachunguzwa ni Lameck Machuki Nyariki (Mkurugenzi wa Nyumba na Mipango), Peris Mose (Mkurugenzi wa barabara na uhasibu), Asberth Maobe (Afisa Mkuu wa Fedha) na Josephat Ouru (Afisa Mkuu wa Barabara na Uchukuzi).
Wachunguzi wanasema maafisa hawa walitekeleza kazi muhimu katika kuidhinisha malipo hayo.
EACC inasisitiza kuwa uvamizi huo unalenga kupata pesa za umma lakini wandani wa Bw Nyaribo nao wamedai analengwa kisiasa.
“Ni njama tu ya kumnyamazisha Gavana Nyaribo kwa sababu ni mwandani wa Dkt Fred Matiangí. Inashangaza kwa sababu uvamizi unakuja siku mbili tu baada ya gavana kuandamana na Dkt Matiangí kutembelea kaburi la Raila Odinga, eneo la Bondo,” akasema Diwani wa Riogoma Nyambega Gisesa.