Makanga 4 ndani kwa kumdunga mwenzao wakipigania abiria
MAKANGA wanne wamefikishwa kortini kwa kumuua mwenzao kwa kumdunga kisu wakipigania abiria.
Hannington Oloo Ogumbo, Duncan Ochola, Vitalis Owino na Daniel Ochieng Ojwang wa kampuni ya Obamana Link wameshtakiwa kwa kumuua Dickson Otieno Ombaka wa Obamana Sacco.
Afisa wa polisi anayechunguza kisa hicho Konstebo Pwoka Mauku aliomba makanga hao wazuiliwe siku 21.
Ogumbo, Ochola, Owino na Ojwang wanadaiwa walimshambulia Ombaka kwa visu na kumuua papo hapo.
Nduguye marehemu, David Omondi Ombaka alifika katika steji ya Temple Road karibu na kituo cha zamani cha mabasi cha OTC ambapo magari ya Obamana hupakia abiria na kujulishwa kisa hicho.
Omondi alifufululiza hadi kituo cha polisi cha Kamkunji na kupiga ripoti.
Aliandamana na polisi hadi Hospitali Medicins Sans Frontier (MSF) iliyoko eneo la Juja ambapo Otieno alipelekwa kupokea matibabu.
“Tulipofika hospitali Otieno alikuwa amekata Kamba,” Mauka alimweleza hakimu.
Aliomba makanga hao wanne wazuiliwe kwa siku 21 ndipo wapelekwe kupimwa akili na mashahidi kuandikisha taarifa kabla ya kupelekwa mahakama kuu kufunguliwa shtaka la kumuua Otieno kinyume cha sheria nambari 203 na 204 za sheria za Kenya.
Ekhubi aliamuru makanga hao wazuiliwe hadi Agosti 8 atakapoamua iwapo atawaacha kwa dhamana ama ataagiza wazuiliwe kwa siku 21 kusaidia ukamilishaji wa uchunguzi.
Hakimu alielezwa washukiwa hao walijisalimisha kwa polisi walipojua wanasakwa kwa kumshambulia na kumuua Otieno.