Makanisa yaunga mkono serikali kudhibiti pombe ‘ili kuokoa kizazi cha sasa’
VIONGOZI wa kidini nchini wametangaza kuwa wanaunga mkono sheria zilizopendekezwa kudhibiti uuzaji wa pombe, wakisema zitafanikisha vita dhidi ya ulevi na kuokoa kizazi cha sasa.
Muungano wa Makanisa na Wahubiri nchini (KCCAM) pia umeitaka serikali ishirikiane nao ili kutekeleza sheria hizo kikamilifu iwapo zitapitishwa.
Askofu wa Kanisa la Deliverance, Geoffrey Njuguna, alisema wako tayari kutumia Neno na vita vya kiroho kupambana na ulevi nchini huku akieleza matumaini kuwa sheria hizo zitapitishwa na hatimaye kutekelezwa.
Hata hivyo, askofu huyo alisema sheria hizo hazifai kutumiwa kuendeleza unyanyasaji na kuwatajirisha watu wachache.
“Mzigo ambao umetwikwa wazazi, shule, uchumi na idara ya afya kutokana na ulevi wa kupindukia, ni jambo lisilopingika. Hatua ya serikali ingekuja mapema ili kuokoa kizazi kinachoangamia,” akasema Askofu Njuguna.
Hivi majuzi serikali ilipendekeza sera ya kupandisha umri ambao mtu anaruhusiwa kunywa pombe kutoka miaka 18 hadi 21.
Pia kuna mapendekezo mengine ya kisheria yaliyotolewa kupitia Sera ya Kitaifa ya Kuzuia, Kusimamia na Kudhibiti Uuzaji wa Pombe na Dawa Nyingine za Kulevya.
Kwenye sheria hizo, serikali ilizima uuzaji wa pombe kwenye fuo, maeneo ya kuvinjari, supamaketi, maduka, mitandaoni na kwenye magari ya uchukuzi.
Unywaji wa pombe pia ulipigwa marufuku kwenye mikahawa na taasisi za masomo.
Tafiti ambazo zimekuwa zikifanywa na mashirika mbalimbali zimeonyesha kuwa matineja huanza kunywa pombe hata wakiwa na umri wa miaka saba pekee.
Kwa mujibu wa KCCAM, familia nyingi zimesambaratishwa, zinakabiliwa na changamoto za kiuchumi pamoja na shida za afya kutokana na uraibu wa pombe pamoja na mihadarati.
KCCAM ilisema uraibu wa pombe na mihadarati miongoni mwa vijana umevuruga maadili yao.
Msimamo wa kanisa unajiri baada ya Waziri wa Usalama Kipchumba Murkomen kuyashutumu kuwa yalikaa kimya na kukosa kujitokeza kuunga mkono pendekezo la kukabili unywaji pombe ambao wamekuwa wakilalamikia unatokomeza jamii.
“Sijasikia kiongozi yeyote wa kanisa akisimama na kusema anaunga mkono sera hii. Hawajaongea ilhali wao ndio huhubiri kuhusu kuwalinda vijana dhidi ya ulevi na matumizi ya dawa za kulevya,” akasema Bw Murkomen, Ijumaa wiki jana akiwa Kaunti ya Kajiado.
Bw Murkomen alisema makanisa yamekuwa mstari wa mbele kuhuburi kuhusu maadili na yanastahili kuunga juhudi za kuwalinda Wakenya dhidi ya ulevi na uraibu wa dawa za kulevya.
Ingawa hivyo, KCCAM ilionya kuwa kuna mwenendo ambao umekuwa ukishuhudiwa ambapo sheria nzuri kama hii hutumiwa na wakora kusaka pesa.
Viongozi wa makanisa kwa hivyo walitaka utoaji wa leseni na mwongozo wa kisheria uwe na uwazi na kujiepusha na ufisadi na unyanyasaji.
Pia walitaka serikali kupigia debe pendekezo hili la sera na kurejelea mahamasisho kwa vijana kuhusu athari ya unywaji pombe pamoja na kukumbatia mipango ya urekebishaji tabia hasa kwa wale ambao tayari wameingiwa na uraibu.
“Sera hii isiwe tu ya kubadilisha sheria ila ilenge kurejesha hadhi, nia na maadili kwa kizazi cha sasa ambacho kinaelekea kuangamia. Tunatoa wito kwa wizara ya Usalama wa Ndani, Mamlaka ya Kupambana na Dawa za Kulevya (NACADA) na mashirika mengine yatekeleze sera hii kwa uwazi,” akasema Askofu Kepha Omae mwenyekiti wa KCCAM.
Askofu Phillip Kitoto wa makanisa ya kievanjelisti pia aliunga mkono sheria za kudhibiti uuzaji pombe akisema zitawaokoa vijana.
Baada ya serikali kutangaza sherehe hizo wiki jana, aliyekuwa Naibu wa Rais Rigathi Gachagua alisema sera au sheria si hoja kwa sababu zimekuwepo lakini kibarua kimekuwa utekelezaji.
“Hizi ni drama ambazo hazitasaidia. Tuna sheria na mwongozo kuhusu pombe. Zitekelezwe na muwaepushe Wakenya na vitimbi hivi, badala yake fanyeni kazi,” akasema Bw Gachagua.