Habari

Malalamishi tele bonasi ya majani chai ikipungua

Na VITALIS KIMUTAI September 29th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

MALALAMISHI mengi yameibuka kuhusu utofauti mkubwa wa viwango vya malipo ya bonasi yatakayotolewa na kampuni 77 za majani chai zinazosimamiwa na Shirika la Ustawishaji wa Majani Chai Nchini (KTDA).

Wakulima kutoka eneo la Mashariki mwa Bonde watapokea malipo ya kati ya Sh26 na Sh57 kwa kilo, kulingana na stakabadhi ambazo Taifa Leo iliona na kuthibitishwa na KTDA.

Kwa upande mwingine, viwanda vilivyoko Magharibi mwa Bonde vitawalipa wakulima bonasi ya kima cha kati ya Sh10 na Sh32 kwa kila kilo ya majani chai, malipo ya chini ikilinganishwa na yale ya mwaka jana.

Kulingana na jinsi KTDA imegawanya maeneo ya kilimo cha majani chai, Mashariki mwa Bonde yanawakilisha kaunti za eneo pana la Mlima Kenya huku Magharibi mwa Bonde likijumuisha maeneo ya Rift Valley na Nyanza Kusini.

Utofauti huu, na kupungua kwa viwango vya malipo ya bonasi mwaka huu ikilinganishwa na mwaka uliopita, umewakasirisha wakulima ambao sasa wanataka maelezo kutoka kwa usimamizi wa KTDA.

Kwa wastani, malipo ya wakulima katika maeneobunge 21 ambako majani chai yanakuzwa yamepungua kwa kati ya Sh0.80 na Sh19.10 kulingana na ripoti ya taarifa ya kifedha ya mwaka uliokamilika Juni 30, 2025.

Wakulima wanaopeleka zao lao kwa Kiwanda cha Majani Chai cha Kiru ndio walioathirika zaidi kwani watalipwa Sh32 kwa kilo ikilinganishwa na Sh51.10 mwaka jana – punguzo la Sh19.10.

Kampuni ya Majani Chai ya Rukuriri ndio inaongoza kwa kulipa Sh57.50 kwa kilo japo malipo hayo yamepungua kwa Sh4 kutoka Sh61.50 iliyotoa mwaka jana.

Kiwanda cha Mununga kinafuata kwa kulipa Sh57 kwa kilo ikilinganishwa na Sh62.65 ilizowalipa wakulima mwaka jana, kuashiria punguzo la Sh5.65.

Kiwanda cha Majani chai cha Imenti kitalipa Sh56 kwa kila kutoka Sh60.30 mwaka jana, punguzo la Sh4.30.

Kwa upande mwingine, wakulima wanaowasilisha majani chai katika kiwanda cha Kiamokama/Rianyamwamu watapokea malipo duni zaidi ya Sh10 kwa kilo ikilinganishwa na malipo ya Sh20 mwaka jana.

Kiwanda cha Nyamache/Itumbe nacho kitalipa Sh11, kutoka Sh20 mwaka jana.

Viwanda vingine vilivyo eneo la Magharibi mwa Bonde kama vile Ogembo/Eberege, Sanganyi, Nyansiongo, Mogogosiek, Kobel na Boito — kila moja vitalipa wakulima wa majani chai Sh12 kwa kilo.

Navyo viwanda vya majani chai vya Gianchore, Kebirigo, Tombe, Kapkoros, Tirgaga, Olenguruone na Motigo will vitalipa bonasi ya Sh13 kwa kilo.

Kiwanda cha Majani chai cha Momul kinacholipa pesa nyingi zaidi katika eneo la Magharibi mwa Bonde kitalipa Sh32 kwa kilo kutoka Sh50.10 mwaka jana, punguzo la Sh18.10.

“Tatizo la utofauti kubwa katika malipo kati ya viwanda katika maeneo ya Magharibi na Mashariki mwa Bonde, ambao umeshuhudiwa kwa miaka kadhaa sharti lishughulikiwe ili kuondoa madai kuwa kuna ukora fulani unaoendelea katika Mnada wa Majani Chai Mombasa,” akasema Cheruiyot Baliach, mkurugenzi wa KTDA wa ngazi ya kanda anayewakilisha Zoni ya Kaptebenget zone katika Kapset/Rorok, Kaunti ya Bomet.