Habari

Mapenzi ya mauti yazidi nchini

April 16th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na WAANDISHI WETU

WAKENYA wamezidi kutamaushwa na visa vingi vya wanawake wanaoangamizwa na wapenzi wao kinyama.

Huku mshukiwa wa mauaji ya Bi Ivy Wangechi akifikishwa mahakamani Jumatatu, mauaji mengine mawili yalitokea na wanawake wawili wakanusurika kifo baada ya kudungwa visu mara kadhaa na wapenzi wao usiku wa kuamkia jana.

Mahakama iliagiza Bw Naftali Kinuthia azuiliwe katika kituo cha polisi cha Naiberi mjini Elodret kwa siku 14 ili kuandikisha taarifa, aendelee kupokea matibabu na pia kufanyiwa uchunguzi wa kiakili kabla ya kufunguliwa mashtaka ya mauaji.

Katika eneo la Nyaribo, Kaunti ya Nyeri, mwanamke mwenye umri wa miaka 24 alidungwa kisu akafariki saa saba usiku wa kuamkia jana baada ya kuzozana na mpenzi wake waliyekuwa wameachana.

Ilisemekana mwanamume huyo alimtafuta na alipomkuta nyumbani kwa rafiki ya mwanamke huyo, alimdunga kisu shingoni.

“Alitoroka baada ya kitendo hicho na tunamtafuta,” Kamanda wa Polisi wa Kaunti Ndogo ya Nyeri ya Kati, Bw Paul Kuria alisema.

Katika kaunti iyo hiyo, mwanamke mwingine mwenye umri wa miaka 30 alilazwa hospitalini baada ya kudungwa kisu mara 17 na mume wake wikendi. Mwanamume huyo baadaye alijisalimisha kwa polisi ambako anazuiliwa.

Kisa sawa na hiki kilitokea katika Kaunti ya Kilifi wakati mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Pwani alidungwa kisu mara kadhaa.

Bi Naomi Chepkemoi alipata majeraha hayo alipozozana na mwanamume anayesemekana wana mtoto naye, nyumbani kwake mjini Kilifi.

Kamanda wa Polisi wa Kaunti ya Kilifi, Bw Patrick Okeri alisema kuwa mshukiwa alisafiri kutoka Nairobi siku ya Jumapili akitaka kujua ni kwa nini mpenzi wake huyo alimrudishia Sh3,200 alizokuwa amemtumia wiki iliyopita kwa minajili ya matumizi ya ulezi wa mtoto wao.

“Maafisa wetu wa polisi waliitwa na majirani na walipofika, mshukiwa alifunga mlango wa nyumba. Ilibidi polisi waingie kwa lazima kumwokoa mwanamke huyo,” akasema Bw Okeri.

Katika hali inayosikitisha zaidi, mwili wa msichana wa darasa la nane ulipatikana umetupwa kichakani jana baada ya kutoweka Jumapili jioni katika Kaunti ya Kisii.

Polisi wangali wanachunguza kisa hicho ingawa ilisemekana marehemu Shylee Mokeira alikuwa amepokea vitisho kutoka kwa mvulana ambaye ni jirani yao awali.

“Nilimsubiri binti yangu aniletee ng’ombe lakini hakurudi ndipo nikaamua kumtafuta. Nilipofika mahali ng’ombe walikuwa, hakuwepo. Nilijaribu kumwita lakini hakuitika. Niliingia ndani ya msitu wa KARI ili nione iwapo aliingia humo kujisaidia. Mtoto wangu hajawahi kukaa nje hadi usiku. Tuliogopa kuingia ndani ya msitu kwa sababu kulikuwa na giza na mvua ilikuwa inanyesha,” akasema mamake, Bi Evaline Nyanchama.

Naibu Kamanda wa Polisi katika Kaunti hiyo Caleb Matoke alisema kwamba msichana huyo aligongwa na kifaa butu kichwani na nguo zilikuwa zimelowa damu.

Tangu mwaka huu ulipoanza, kumekuwa na visa visivyopungua kumi vya aina hii ambavyo vimeripotiwa na inahofiwa kuwa kuna vingine vingi ambavyo huenda havifikii wanahabari.

Miongoni mwavyo ni vile vilivyohusu mauaji ya Bi Beryl Adhiambo Ouma aliyeuawa katika mtaa wa Kahawa Sukari, Nairobi na Bi Beryl Atieno wa Ndhiwa, Kaunti ya Homa Bay.