Habari

Maraga afungua mahakama ya kisasa Nakuru

December 5th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na RICHARD MAOSI

JAJI mkuu David Maraga siku ya Ijumaa, aliongoza hafla ya kufungua mahakama ya kisasa Nakuru kama njia ya kutoa nafasi kushughulikia kesi nyingi kwa wakati mmoja.

Maraga aliandamana na msajili mkuu wa mahakama Ann Amadi, Gavana wa Nakuru Lee Kinyanjui miongoni mwa viongozi wengine.

Katika hotuba yake Maraga alisema mahakama hii mpya itasaidia kupunguza mrundiko wa kesi na kuboresha huduma za mahakama kwa raia.

Aidha aliongezea kuwa mahakama ya Nakuru ina seli tofauti kwa jinsia ya kike na ile ya kiume mbali na kuwa na ofisi za kutoa huduma ya Ofisi ya Kiongozi wa Mashtaka , mawakili na majaji.

“Isitoshe kuna vyumba vinane vya kutoa hukumu na vizimba 12 kwa washtakiwa kusimama wakati wa kusikiliza hukumu,” akasema.

Aidha wahudumu wa kortini wana sehemu ya kubarizi baada ya kazi, pamoja na sehemu ya akina mama kuwanyonyeshea watoto wao.

Aidha mtandao umeunganishwa kila sehemu na sehemu zenye runinga kwa wakazi kufuatilia kesi za jamaa zao au hata marafiki.

Alipendekeza kesi kuhifadhiwa katika faili za mtandao ili kupunguza visa ambapo faili za walalamishi kupotea katika njia isiyoweza kueleweka.

Jaji Mkuu David Maraga (wa pili kulia) baada ya kufungua mahakama mpya ya kisasa katika Kaunti ya Nakuru. Aliandamana na Gavana wa Nakuru Lee Kinyanjui na msajili mkuu wa mahakama Ann Amadi. Picha/ Richard Maosi

Alisema pia kuzingatia mfumo wa teknolojia katika hatua ya kufuatilia kesi kutasaidia kupambana na visa vya ushahidi wa kesi kupotea.

Hata hivyo Maraga alisema kuwa mahakama imekuwa ikipata changamoto kutokana na idadi kubwa ya vijana wadogo wengine chini ya umri wa miaka 20 wanaotiwa gerezani kutokana na mashataka ya ubakaji.

“Vijana wengi ambao bado ni wadogo wamekuwa wakitiwa gerezani kwa miaka mingi, hali ambayo inatujuzu sisi kama idara ya mahakama kufikiria upya kuhusu sheria hizi kali ambazo zimekuwa zikiwalemea wavulana,” akasema.

Maraga alishukuru Benki ya Dunia kwa kuwa mfadhili mkuu wakati wa kutengeneza mahakama hii ya kipekee katika eneo la Bonde la Ufa.

Hivi karibuni idara ya mahakama imefanikiwa kujenga mahakama kuu nne katika kaunti za Isiolo, Vihiga, Kwale na kaunti ya Nandi na kufikisha idadi ya mahakama kuu 43 kati ya kaunti 42, Kaunti ya Nkuru ikiwa ni mojawapo ya kaunti yenye zaidi ya mahakama kuu mbili.

Kaunti za Samburu, Wajir na Elgeyo Marakwet ndizo hazina mahakama kuu.