Marufuku ya Waziri Kagwe kuhusu macadamia yasambaratisha bei
BEI ya zao la macadamia ilishuka kutoka Sh150 hadi Sh90 kwa kilo baada ya Waziri wa Kilimo Mutahi Kagwe kurejesha marufuku dhidi ya uuzaji wa macadamia mabichi.
Hatua hiyo ambayo Wizara ilichukua mnamo Februari 27, mwaka huu ilichangia wakulima wengi kupata hasara kubwa.
Mmoja wao, Josephat Muriira kutoa Meru sasa anakadiria hasara baada ya tani moja aliyovuna kukosa kumletea mapato aliyotarajia.
“Nimepoteza Sh60,000 kufuatia tangazo hilo la Waziri Kagwe,” anasema Bw Muriira ambaye ni mwenyekiti wa wakulima wa Macadamia katika eneo bunge la Tigania Magharibi.
“Wizara hiyo ingetupa angalau notisi ya muda fulani ili tuweze kuzuia hasara. Tulipowekeza katika mashamba yetu hatukujua kuwa ilikuwa ni mchezo wa kamari,” akasema.
Masaibu ya Bw Muriira pia yamewasibu wakulima wengine wa macadamia katika kaunti za Meru, Murang’a na Nyeri.
Wakulima hao walikuwa wakidhani kuwa hali ingekuwa kama ilivyokuwa Novemba 2023 wakati ambapo Wizara ya Kilimo iliondoa marufuku dhidi ya kuuza macadamia mabichi katika masoko ya kimataifa.
Marufuku hiyo ilikuwa imewekwa mnamo 2009.
Nafasi hiyo ya uuzaji macadamia yasiyokaushwa katika masoko ya kimataifa ilifikia kikomo mnamo Novembea 2024.
Mwezi jana, Waziri Kagwe alisema serikali itahakikisha kuwa marufuku hiyo imetekelezwa kulingana na Sheria ya Mamlaka ya Kilimo na Chakula (AFA) na Kanuni kuhusu Mazao ya Mafuta ya 2020.
“Tunawahimiza wakulima kujisajili kwenye mfumo wa pamoja wa kuhifadhi data kuhusu kilimo (KIAMS) ili kutuwezesha kuweka mipango na kutoa usaidizi hitajika,” akasema.