HabariHabari za Kaunti

Masaibu ya Mwangaza yagawanya Njuri Ncheke

Na DAVID MUCHUI August 10th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

MZOZO wa kisiasa katika Kaunti ya Meru kuhusu kuondolewa mamlakani kwa Gavana Kawira Mwangaza umegawanya Baraza la wazee la Njuri Ncheke.

Wiki iliyopita, kundi pinzani liliibuka kumtetea Gavana Mwangaza na likachagua viongozi akiwemo Adrian Aruyaru (Mwenyekiti) na Solomon Kinyua (Katibu Mkuu).

Bw Aruyaru, ambaye alikuwa shahidi wa upande wa utetezi wakati wa kuondolewa kwa Bi Mwangaza katika Seneti mwaka jana, aliongoza zaidi ya wazee 500 kutimua Mwenyekiti Linus Kathera na katibu mkuu Josphat Murangiri.

Chimbuko la mgawanyiko huo ni matukio ya Oktoba 14, 2023 wakati wa kilele cha mchakato wa kumwondoa madarakani Gavana Mwangaza kwa mara ya tatu.

Wakati huo, Njuri Ncheke ilimteua aliyekuwa Waziri wa Kilimo Mithika Linturi, kuwa msemaji wa Ameru na kutoa baraka kwa Naibu Gavana Isaac Mutuma na kuwalisha kiapo madiwani kuunga mkono mchakato wa kumtimua.

Baada ya tukio hilo Bw Aruyaru aliwashutumu Bw Kathera na Bw Murangiri kwa kuvunja sheria na kanuni za baraza hilo.

Hata hivyo, ni jaribio la hivi punde la kumuondoa Bi Mwangaza ambalo lilichochea mapinduzi ambayo sasa yameiacha Njuri Ncheke kuwa na mirengo miwili.

Akizungumza na Taifa Leo, Bw Aruyaru alisema waliamua kuchukua uongozi wa Njuri Ncheke baada ya viongozi wao kukataa agizo la Mahakama Kuu la kuwapatanisha gavana na madiwani.

“Viongozi wetu wamedhalilisha jina zuri la Njuri Ncheke kwa kuunga mkono upande mmoja na kukataa agizo la mahakama. Hakuna kesi ngumu sana kwa wazee wa Njuri Ncheke. Tumechukua nafasi ili kuokoa jina la baraza,” Bw Aruyaru alisema.

Lakini Bw Kathera alimshutumu Bw Aruyaru akisema alifanya uchaguzi na hafla isiyo halali katika makao makuu ya Njuri Ncheke.