Masaibu yaendelea kuandama biashara za familia ya Joho
BIASHARA za familia ya Waziri wa Madini na Uchumi wa Majini, Bw Ali Hassan Joho zimeathirika na maamuzi ya mahakama kiasi cha kurejesha nyuma ufanisi wake nchini na eneo la Afrika Mashariki.
Kwa mfano, maamuzi ya mahakama yametisha kuvuruga ushawishi wa familia hiyo katika biashara ya uchukuzi na upakuaji bidhaa bandarini.
Kampuni ya Autoport Freight Terminals & Portside Freight Terminals imekuwa ikijaribu kutawala biashara ya usimamizi wa shughuli za bandari na uchukuzi wa mizigo kutoka Mombasa hadi Nairobi na hata hadi jiji la Juba nchini Sudan Kusini.
Lakini hali imebadilika pakubwa katika miezi michache iliyopita kutokana mapigo ambayo biashara za familia ya Joho zilipata kutokana na maamuzi ya asasi za serikali kwa upande mmoja na maagizo ya Mahakama Kuu na Mahakama ya Juu, kwa upande mwingine.
Kwa mfano, Agosti 2023, Wizara ya Uchukuzi na Mamlaka ya Ushuru Kenya (KRA) iliruhusu kampuni nyingine kushiriki katika shughuli za usafirishaji wa mizigo hadi Sudan Kusini.
Kabla ya hapo, kampuni ya Autoport Freight Terminals, ya kaka wa Joho, Abu Joho, ndiyo ya kipekee iliyokuwa ikisafirisha mizigo kutoka bandari ya Mombasa hadi Sudan Kusini.
Wakati huo, Bw Joho, ambaye ni mwandani wa kiongozi wa ODM Raila Odinga hakuwa akielewana na Rais William Ruto, ambaye alikuwa ameingia afisi Septemba 13, 2027.
Katika barua iliyoandikwa na Katibu wa Wizara ya Uchukuzi Mohamed Daghar mnamo Julai 25, 2023, afisa huyo aliteua kampuni zingine tatu Compact Consolbase, Mombasa Container Terminal, na Mitchell Cotts, kusafirisha tani 1.1 milioni za mizigo kati ya Mombasa na Sudan Kusini.
Uamuzi huo uliathiri pakubwa ukiritimba wa kampuni ya Autoports katika biashara hiyo ya thamani ya mabilioni ya pesa.
“Waagizaji bidhaa na wenye mizigo kutoka Sudan Kusini wako huru kuteua kampuni yoyote iliyoidhinishwa na KRA,” akaandiki Bw Daghar kuashiria kuwa serikali ya Kenya haingeelekeza uteuzi wa kampuni ya kupitisha na kusafirisha mizigo.
Hatua hiyo ya kuiweka sekta hiyo huria ilitokana na presha kutoka kwa mataifa ya kanda hii ambayo hayakuridhishwa na huduma mbaya ya Autoport, ikiwemo kucheleweshwa kwa mizigo.
Kampuni hiyo ilipokuwa akitafakari kuhusu pigo hilo, pigo kubwa la kisheria lilitokea mnamo Juni 2025.
Hii ni baada ya Mahakama ya Juu kutupilia mbali uamuzi ambao ulikuwa umeipa kampuni ya Portside Freight Terminals, kampuni nyingine ya familia ya Joho, kibali cha kujenga bohari nyingine la nafaka katika bandari ya Mombasa.
Mahakama ya Juu iliamua kuwa Mamlaka ya Bandari Nchini (KPA) ilikuwa imekiuka sheria husika ilipoipa kampuni hizo zabuni ya kujenga bohari hilo.
Majaji walibaini kuwa KPA, kimakusudi ilikataa kutangaza wazi zabuni hiyo ili ishindaniwe na kampuni zingine.