Habari

Maseneta wachemkia wabunge kwa kukosa kuwahusisha kukagua maafisa IEBC

Na COLLINS OMULO May 19th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

HUENDA maseneta na wabunge wakatofautiana vikali kuhusu mchakato wa kuwapiga msasa makamishina wateule wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) ulioratibiwa kufanyika wiki hii.

Hii ni baada ya maseneta kulalamikia kutohusishwa kwao katika shughuli hiyo ambayo wabunge wanasema ni wao pekee ambao sheria inawaruhusu kuendesha.

Maseneta wanalitaka Bunge la Kitaifa kuondoa ilani iliyochapishwa kualika Wakenya kuwasilisha memoranda za kupinga uidhinishaji wa wateule hao, wakidai siyo halali bila kushirikishwa kwa Seneti katika shughuli hiyo.

Wanashikilia kuwa uteuzi wa mwenyekiti na makamishna wa IEBC ni suala lenye umuhimu wa kitaifa, kwani unahusisha viwango viwili vya serikali-na hivyo sharti ihusishwe mabunge yote mawili.

Kauli hiyo huenda ikafufua vita vya ubabe katika Bunge la Kitaifa na Seneti.

Mnamo Mei 27, Kamati ya Bunge la Kuhusu Haki na Masuala ya Sheria (JLAC) imeratibiwa kuanza kuwapiga msasa mwenyekiti mteule wa IEBC Erustus Ethekon na makamishna sita wateuliwa, bila kuhusisha Seneti.

Kutohusishwa huko kumewakasirishwa maseneta wanaoshikilia kuwa shughuli hiyo sharti iendeshwe na mabunge hayo mawili ilivyofanyika kwa maafisa wengine wakuu wa serikali.

Mwenyekiti wa Kamati ya Seneti kuhusu Haki na Masuala ya Kisheria Hillary Sigei alirejelea shughuli awali za aina hiyo—ikiwemo kupigwa msasa kwa Inspekta Jenerali, Gavana wa Benki Kuu na Makamishna wa Tume ya Ugavi wa Mapato (CRA)- ambapo mabunge hayo mawili yalishiriki kupitia kamati za pamoja za JLAC.

Ilivyo sasa, Kipengele cha 250 (2) cha Katiba na Sheria ya IEBC ya 2024 zinasema kuwa makamishina wateule wa IEBC watapigwa msasa na Bunge la Kitaifa.

Kulingana na kipengele hicho, baada ya kupokea majina hayo, Bunge la Kitaifa litawapiga msasa na kuwaidhinisha au kuwakataa wateule hao.

Hata hivyo, Bw Sigei anasema kuwa sehemu husika ya sheria ya IEBC kuhusu suala hilo ilifanyiwa marekebisho mnamo 2012, kabla ya Seneti kuundwa rasmi.

Aliongeza kuwa hitaji kwamba bunge la kitaifa ndilo lenye jukumu la kupiga msasa wateule wa IEBC lilipasa kutumika katika uchaguzi mkuu wa kwanza, pekee, baada ya kuzinduliwa kwa Katiba ya sasa.

“Kwa hivyo msimamo wetu ni kwamba, mchakato huu wa kuwapiga msasa makamishina wateule wa IEBC unapasa kuendesha, kwa pamoja, na mabunge yote mawili jinsi inayofanyika kwa uidhinishaji wa teuzi za washikilizi wa Afisi Kuu za Serikali,” Bw Sigei akasema.

“Badiliko hili, ambalo liliweka jina nafasi ya neno “Bunge” iliweka jina “Bunge la Kitaifa” lilinuiwa kutumika katika awamu ya mpito. Tangu wakati huo Bunge la Kitaifa limehujumu juhudi zetu na kurejesha neno “Bunge” katika sheria,” akaongeza Bw Sigei ambaye ni Seneta wa Bomet.

Seneta huyo alisema pendekezo la Seneti la kutaka kurejesha neno hilo “Bunge” lingali katika Bunge la Kitaifa.

“Kwa ukweli hii ni mmoja ya Miswada ambayo Bunge la Kitaifa limekalia kwa muda mrefu kupita kiasi na kinyume na inavyotakikana. Ningependa kuweka wazi kwamba kama kamati ya JLAC katika Seneti hatutaachilia pendekezo hili,” akaeleza.