Maseneta wapinga mapendekezo ya Ruto kukabili ufisadi serikalini
JITIHADA za Rais William Ruto kuanzisha sheria kali za kupiga vita ufisadi zimepata upinzani mkali katika Seneti, ambapo maseneta wanapinga vipengele viwili muhimu vya Mswada tata wa Migongano ya Maslahi wa 2023.
Maseneta wameelezea kutoridhishwa kwao na kipengele kinachotaka watumishi wa umma kutangaza zawadi wanazopokea wao au jamaa zao ndani ya saa 48, pamoja na tafsiri pana ya neno “jamaa,” hasa matumizi ya neno “uhusiano wa karibu”.
Mswada huo unalenga kuweka adhabu kali dhidi ya watumishi wa umma wanaofanya biashara na serikali kwa kutumia nafasi zao kujitajirisha, tabia ya ufisadi ambayo imewageuza baadhi kuwa mamilionea ghafla licha ya mishahara yao midogo isiyoendana na maisha yao ya kifahari.
Tangu upitishwe na Bunge la Kitaifa mwezi Novemba 2023 na baadaye na Seneti mwezi Juni 2024, mswada huu umepitia mabadiliko mengi yaanayovuruga madhumuni yake ya awali, jambo lililomfanya Rais kukataa kuutia saini.
Rais Ruto alipinga vipengele 12 ambavyo alisema vililegezwa na Bunge, ikiwa ni pamoja na kifungu ambacho kinaeleza “jamaa” kuwa mtu aliye na uhusiano na mtumishi wa umma kwa njia ya damu, ndoa, kuasili au kihisia.
Rais anasisitiza kuwa ni muhimu kuweka tafsiri hiyo ili kuzuia watumishi wa umma kutumia jamaa zao kuficha mali yao, na hivyo kuhujumu mifumo ya uwajibikaji.
Hata hivyo, maseneta wanapinga matumizi ya neno ” ukaribu,” wakisema tafsiri yake ni pana mno, isiyoeleweka wazi, na inaweza kutumiwa kisiasa kuonea watu.
Seneti inahitaji thuluthi mbili (maseneta 45 kati ya 67) ili kukataa marekebisho ya Rais.
Seneta wa Vihiga, Godfrey Osotsi, alisema neno hilo lina utata mkubwa na linaweza kutumiwa kuwakandamiza watu kisiasa.
“Unaweza kuwa na uhusiano wa aina hii na mtu yeyote, hata walioko humu ndani. Kwa kuwa mimi na wewe ni maseneta, ina maana tuna ukaribu. Sasa nikifanya kosa, wewe ushikwe kwa sababu ya mimi? Hili neno litatumika kwa uonevu wa kisiasa,” alisema Bw Osotsi.
Seneta wa Uasin Gishu, Jackson Mandago, alisema neno hilo linapaswa kufutwa kwa kuwa halieleweki vizuri na linaweza kutumiwa vibaya na taasisi za kifedha au kisiasa.
“Hatuwezi kuelewa vizuri lengo la Mswada huu. Tuwe waangalifu, maana baadhi ya taasisi zinazotekeleza sheria zinaweza kutumiwa kisiasa,” aliongeza.
Seneta Maalum Esther Okenyuri alipendekeza Seneti itoe tafsiri mbadala ya maneno “familia,” “jamaa” na “uhusiano wa karibu,” akionya kuwa kutofafanua vyema kunaweza kuwaumiza watu wasio na hatia.
“Tukishindwa kufafanua vizuri tunachomaanisha, tutakuwa tumeweka watu wengi katika hatari kwa kuhusishwa na watu fulani tu kwa kuwa tunawafahamu,” alisema Bi Okenyuri.
Seneta wa Nandi, Samson Cherargei, alisema neno hilo lina hatari kwa kuwa linaashiria kuwa mtu yeyote unayemfahamu kwa karibu anaweza kuchukuliwa kuwa jamaa yako.
“Hii ni ajenda ya Benki ya Dunia na mashirika ya kigeni ambayo hayaelewi tamaduni zetu. Hauwezi kusema kuwa kwa kuwa tumekuwa marafiki, basi tuna ‘uhusiano wa kihisia’,” alisema.
Seneta wa Tana River, Danson Mungatana, alisema utekelezaji wa kipengele hicho utakuwa mgumu kwa sababu neno hilo ni pana mno.
“Ina maana kuwa wakitaka kumchunguza mtumishi wa umma, wanaweza kuwafuata watu wanaohusiana naye kwa hali yoyote ya ukaribu au urafiki. Hii ni kinyume na haki ya kikatiba ya kushirikiana na wengine,” alisema.