Habari

Maseneta wataka EACC imulike serikali nzima ya Natembeya

Na COLLINS OMULO September 24th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

MASENETA wanataka Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) kupanua uchunguzi wake katika Kaunti ya Trans Nzoia ili kujumuisha ukusanyaji mapato, kufuatia madai ya “wizi wa mapato” unaoonekana kuwa wa kimfumo katika serikali hiyo.

Haya yanajiri baada ya Gavana George Natembeya kukiri kuwepo kwa mianya na wizi wa mapato yanayokusanywa na serikali ya kaunti yake.

EACC tayari inachunguza miradi kadhaa ya mamilioni ya pesa inayoendelezwa na serikali ya kaunti hiyo ambayo imezua maswali.

Alipofika mbele ya Kamati ya Bunge la Seneti ya Hesabu za Umma za Kaunti Jumanne, Gavana Natembeya alikiri kwamba kuna uwezekano wa watu kukusanya pesa na kuweka mfukoni badala ya kuwasilisha kwa serikali ya kaunti.

Hii ni baada ya ripoti ya kaunti kuonyesha kuwa Sh261 milioni pekee zilikusanywa kutoka kwa vyanzo mbalimbali vya mapato (isipokuwa ada za hospitali), ilhali lengo lilikuwa Sh643 milioni.

Kwa mujibu wa Tume ya Ugavi wa Mapato (CRA), uwezo wa kaunti hiyo kukusanya mapato kutoka kwa vyanzo vyake binafsi ni angalau Sh2 bilioni.

Licha ya serikali ya kaunti kubadilisha mfumo wake wa ukusanyaji mapato, kamati inayoongozwa na Seneta wa Homa Bay Moses Kajwang’ ilielezwa kuwa kaunti hiyo bado ilikumbwa na upungufu wa Sh22.7 milioni katika mwaka wa kifedha ulioishia Juni 30, 2024.

Katika kipindi hicho, vyanzo 11 vya mapato vilirekodi kupungua kwa mapato licha ya serikali ya kaunti kutumia Sh26 milioni kununua mfumo mpya wa ukusanyaji mapato.

Katika mfano mmoja, serikali ya kaunti iliripoti kukusanya Sh38,000 pekee kutoka kwa vichinjio kwa mwaka mzima.

Kwa mujibu wa Gavana, gharama ya kuchinja ng’ombe mmoja ni Sh40, hivyo ni kana kwamba ni ng’ombe 950 tu waliochinjwa katika vichinjio vyote vya kaunti kwa mwaka mzima.

“Inaonekana watu wanakusanya pesa na kuweka mifukoni. Huu ni mfano wa wizi wa wazi. Zaidi ya Sh20 milioni zimeibwa kutoka kwa watu wa Trans Nzoia. Tunataka kujua ni nani EACC wanapaswa kumfuatilia. Je, ni muuzaji wa mfumo, mkusanyaji wa mapato au gavana?” alihoji Seneta Kajwang’.

“EACC lazima wachunguze ukusanyaji wa mapato Trans Nzoia na watueleze ikiwa pesa zilikuwa zikikusanywa kisha kutoweka. Iwapo pesa hizo hazikuwasilishwa, basi maafisa waliohusika wafunguliwe mashtaka,” aliongeza.

Seneta Kajwang’ alisema kamati hiyo inataka kufahamu ikiwa tatizo liko kwa wakusanyaji wa mapato au mfumo mpya, akieleza kuwa hali hiyo ni ishara ya “wizi wa kimfumo”.

“Hakuna njia Trans Nzoia inakusanya Sh261 milioni pekee bila kujumuisha ada za hospitali, ilhali kaunti ina utajiri mkubwa. Wewe (Natembeya) lazima uhakikishe pesa wanazolipa kina mama mboga zinahesabiwa. Zisipohesabiwa, wafukuze wezi,” alisema.

Akiwa amebanwa, Gavana Natembeya alikiri kuwepo kwa tatizo la kupotea kwa mapato katika serikali yake ya kaunti, ambalo alisema anajaribu kulitatua.

Alieleza kuwa uwezo wa kaunti hiyo kukusanya mapato ni Sh800 milioni na tayari wanafunga mianya katika idara ya mapato ili kufikia kiwango hicho.

“Ndio, kuna uwezekano kwamba watu wanakusanya pesa na kuweka mifukoni. Watu wanapigania kupelekwa katika idara ya mapato. Hiyo yenyewe ni ishara kuwa kuna wizi,” alisema Gavana Natembeya.

Hata hivyo, alieleza kuwa kupungua kwa Sh22.7 milioni katika ukusanyaji wa mapato kulitokana kwa kiasi kikubwa na mabadiliko ya mfumo wa ukusanyaji mapato.

Alisema mfumo mpya uliletwa wakati wa kilele cha msimu wa ukusanyaji wa mapato, na kwamba serikali yake haikuweza kukusanya mapato nje ya mfumo huo.