Habari

Maseneta wataka kubuniwe afisi ya kushughulikia usalama wao

September 10th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na CHARLES WASONGA

MASENETA sasa wanaitaka Tume ya Huduma Bunge (PSC) kuanzisha afisi maalum itakayoshughulikia masuala yote yanayohusiana na usalama wao na wabunge ili kukomesha visa vya kukamatwa kwa wajumbe “kwa njia ya aibu”.

Pendekezo hili lilitolewa na Kamati ya Seneti kuhusu Usalama ambayo ilichunguza kisa cha juzi cha kukamatwa kwa maseneta watatu kwa namna ya kutatanisha.

Kulingana na ripoti hiyo iliyowasilishwa Jumanne na mwenyekiti wa kamati hiyo Yusufu Haji, afisi hiyo maalum itashughulikia masuala yote ya kuhusu usalama wa wabunge na maseneta ikiwemo amri za kuwataka kufika mbele ya asasi za kiusalama.

“Ikiwa maafisa wa usalama wanataka wabunge au maseneta wafike mbele yao kuandikisha taarifa au wanataka kuwakamata, watahitajika kushirikiana na afisi hiyo maalum,” ripoti hiyo inasema.

Katika ripoti hiyo, kamati hiyo imewakashifu polisi kuhusu kwa kuwakamata maseneta Cleophas Malala (Kakamega), Steve Lelengwe (Samburu) na Christopher Lang’at “kwa njia ya kikatili na kinyama”.

Watatu hao walikamatwa na maafisa wa Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) katika makazi yao mnamo Agosti 17 walipokuwa wakijiandaa kuhudhiria kikao cha kujadili suala tata la mfumo wa ugavi wa fedha baina ya kaunti.

Walisafirishwa hadi kaunti zao wakaandikisha taarifa kwa kutoka na kile polisi walisema ni uchunguzi ambao umekuwa ukiendelea dhidi yao. Hata hivyo, hawakufunguliwa mashtaka.

Haya yanajiri wakati ambapo Inspekta Jenerali wa Polisi Hillary Mutyambai alikosa kufika mbele ya Kamati hiyo ya Usalama kutoa maelezo kuhusu madai ya Seneta wa Kakamega Cleophas Malala kwamba maisha yamo hatarini.

Spika wa Seneti Kenneth Lusaka aliagiza Kamati hiyo imwite Bw Mutyambai baada ya Bw Malala kumwomba ahakikishe ameongeza walinzi akidai watu fulani wamekuwa wakimfuata kwa nia ya kumdhuru.

Lakini Inspekta Jenerali alisema hangefika mbele ya Seneta Haji na mwenzake siku hiyo “kutokana na sababu za kikazi” na akaomba aruhusiwe kujiwasilisha Jumatatu wiki ijayo.