Maseneta waunga wito wabunge wapokonywe NG-CDF
MVUTANO kuhusu Hazina ya Serikali ya Kitaifa ya Maendeleo ya Maeneo Bunge (NG-CDF) unaendelea kuchacha huku maseneta kadhaa wakiunga mkono wito wabunge wapokonywe usimamizi wa hazina hiyo ikabidhiwe magavana.
Katika matamshi aliyotoa mapema wiki hii, Kiongozi wa ODM, Raila Odinga alisisitiza kuwa NG-CDF haipaswi kuwa mikononi mwa wabunge kwa kuwa serikali za kaunti zimepewa jukumu la kutekeleza miradi ya maendeleo mashinani.
“Hatuwezi kuwa na mfumo wa ugatuzi kisha wabunge washikilie fedha ambazo kikatiba si jukumu lao kuzisimamia. Hazina ya CDF inapaswa kusimamiwa na serikali za kaunti,” alisema Raila katika mkutano wa kisiasa uliofanyika Kisumu.
Kauli hiyo imeungwa mkono na maseneta kadhaa wa ODM akiwemo Seneta wa Migori, Eddy Oketch, ambaye ametaja hazina hiyo kuwa na udhaifu mkubwa wa usimamizi na matumizi mabaya ya rasilimali.
Akizungumza kwenye mahojiano na runinga ya Citizen, Seneta Oketch alisema kuwa ni wakati wa kuwapokonya wabunge usimamizi wa Hazina ya NG-CDF na kuikabidhi magavana ili kuwe na uwajibikaji zaidi.
“Wabunge wanapaswa kujikita katika kazi zao za msingi za kutunga sheria, kuwakilisha wananchi na kupiga darubini serikali. Si jukumu lao kuwa watekelezaji wa miradi ya maendeleo. Fedha za umma zinapokuwa mikononi mwa wanasiasa bila usimamizi huru, mianya ya ufisadi huwa wazi,” alisema Oketch.
Aidha, Seneta wa Kisumu, Profesa Tom Ojienda, ambaye pia ni mtaalamu wa sheria, alisisitiza kuwa uamuzi wa Mahakama Kuu wa mwaka 2016 uliotangaza Hazina ya NG-CDF kutokuwa halali bado upo.
“Hazina hii inakiuka vipengele muhimu vya Katiba kama vile Ibara za 174, 175 na 201 kuhusu ugatuzi na usimamizi wa fedha za umma. Hata baada ya marekebisho yaliyofanywa na Bunge, bado ina dosari kikatiba,” alisema Ojienda.
Kwa mujibu wa Ojienda, iwapo hazina hiyo itahamishiwa rasmi kwa serikali za kaunti kufikia mwaka 2026 kama ilivyoelekeza mahakama, ubunge hautakuwa kivutio tena kwa wanasiasa wanaotegemea fedha hizo kujijenga kisiasa mashinani.
“Uchaguzi unapaswa kutegemea hoja, sera na utendaji, si kwa mgombea kugawa pesa vijijini kupitia hazina za serikali,” aliongeza.
Wabunge wameendelea kuitetea NG-CDF wakisema kuwa imekuwa msaada mkubwa kwa miradi ya elimu, barabara ndogo na maendeleo ya kijamii.
Mgogoro huu unaibuka wakati ambapo Hazina ya Kitaifa imeahidi kutoa Sh 7 bilioni 7 kwa NG-CDF kufuatia malalamishi ya wabunge kuhusu ucheleweshaji wa fedha.
Mbunge wa Mumias Mashariki Peter Salasya anasema magavana hawana uwezo wa kusimamia pesa hizo hasa kuhusiana na ujenzi wa miundomisingi shuleni.
Mbunge wa Kitui Central, Dkt Makali Mulu, alilaumu Raila kwa kupendekeza CDF isimamiwe na magavana.