Habari

Masharti makali yawekwa shule zinapofunguliwa

October 11th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na FAITH NYAMAI

WANAFUNZI sasa watakumbana na hali isiyo ya kawaida watakaporejea shuleni Jumatatu baada ya likizo ya miezi saba iliyosababishwa na janga la Covid-19.

Masharti makali yaliyotangazwa na Wizara ya Elimu yamefanya mazingira ya shule kuwa magumu kwa wanafunzi, kumaanisha kuwa, wanafunzi watalazimika kuzoea hali hiyo mpya huku mafunzo yakiendelea.

Kuanzia langoni hadi kwenye madarasa, vyooni, mabwenini na mazingira mengine ya shuleni, hali imebadilika na wanafunzi watahitajika kuzingatia kikamilifu masharti ya afya.

Watoto hawataruhusiwa kucheza au kutangamana miongoni mwao na wala hawataruhusiwa kutagusana.

Wakuu wa shule tayari wametoa masharti kwa walimu wakiwataka kununua maski zinazoweza kutumiwa kwa muda mrefu kama sehemu ya sare ya shule la sivyo hawataruhusiwa shuleni.

Katika baadhi ya shule za bweni, wanafunzi wameagizwa kuwa shuleni kufikia saa kumi jioni.

Shule pia zimeelekeza wanafunzi kutobeba sanitaiza wakisema zitatolewa na shule huku baadhi za shule zikiruhusu tu chupa za milimita 80.

Shule zote zinahitajika kutoa maji safi katika kiingilio na sehemu za jumla huku wanafunzi wakihitajika kuosha mikono yao kabla ya kuingia lango la shule, kuvalia maski na kufanyiwa vipimo vya joto kila siku.

Mwenyekiti wa Muungano wa Walimu Wakuu wa Shule za Sekondari Kenya (Kessha) Kahi Indimuli alisema shule zinaharakisha kuweka mikakati yote jinsi ilivyoamrishwa na Wizara ya Elimu.

“Tumeshughulikia kujitenga kijamii, kuweka vituo vya maji vya kuoshea mikono na kuzingatia masharti yaliyowekwa tayari kuanza muhula mpya,” alisema Bw Indimuli.

Mwenyekiti mwenzake wa Muungano wa Walimu Wakuu wa Shule za Msingi (Kepsha), Nicholas Gathemia alisema walimu wako tayari kukutana na wanafunzi wao baadsa ya likizo ndefu.

“Kufunguliwa tena kwa shule ni hatua moja zaidi na sisi kama walimu tumekaribisha hatua hiyo kwa sababu walimu wako salama zaidi shuleni kuliko nyumbani,” alisema Bw Gathemia.

Alisema wazazi wanapaswa kuandaa watoto wao na kununua vitu vyote vinavyohitajika ikiwemo maski.

“Ni jukumu la wazazi kuhakikisha watoto wao wanavalia maski la sivyo hawataruhusiwa kuingia shuleni,” alisema Bw Gathemia.

Hata hivyo, alisema wanafunzi kutoka familia maskini huenda wakawa na bahati ya kupatiwa barakoa za serikali zitakaposambazwa shuleni.

Wanafunzi pia hawatashiriki michezo, tamasha za ugizaji na muziki, spoti au tamasha nyingine yoyote inayoweza kusababisha misongamano.

Katika baadhi ya shule, wanafunzi huenda wakalazimika kusomea chini ya miti kutokana na nafasi, wengine wakilazimika kusomea chini ya hema huku shule zikizingatia sheria kuhusu kuepuka kutangama kwa karibu.

Katika baadhi ya maeneo kama vile Baringo, baadhi ya shule zimefurika na vifaa vya shule kuharibiwa hali ambayo huenda ikalazimu wazazi kutafuta shule mbadala.

Shule ya msingi ya mmiliki binafsi ya Mwea Brethren, Kaunti ya Kirinyaga, bado inaendelea na biashara yake ya kufuga kuku.