Masharti ya ODM yakoroga Ruto
RAIS William Ruto amechukua tahadhari kuu huku chama chake, United Democratic Alliance (UDA), kikijaribu kuunda ushirikiano wa kisiasa kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027.
Hali imezidi kuwa mbaya baada ya chama cha Orange Democratic Movement (ODM) kudai wadhifa wa Naibu Rais, jambo ambalo limezidisha kizungumkuti cha kisiasa kwa Rais Ruto.
Katika mahojiano ya kipekee na Taifa Dijitali, kaimu kiongozi wa ODM, Dkt Oburu Oginga, alisema chama chake hakitakubali chochote chini ya wadhifa wa naibu rais katika mpangilio wowote wa muungano — iwe ni pamoja na UDA ya Ruto au upinzani.
“Ikiwa tutalazimika kukubali wadhifa wa chini, haupaswi kuwa chini ya kiti cha pili kwa ukubwa (Naibu Rais) katika muundo wowote. Hilo ndilo nadharia yangu. Hatutakubali chochote chini ya hicho,” alisema Dkt Oginga.
Mwaka mmoja pekee baada ya mzozo wake (Rais Ruto) na aliyekuwa naibu rais Rigathi Gachagua — uliosababisha kutimuliwa kwa Gachagua serikalini Oktoba mwaka jana— dalili za mgongano sasa zinaonekana kati ya viongozi wa Mlima Kenya Mashariki, ambao wamesimama na Profesa Kithure Kindiki kuwa mgombea mwenza wa Ruto 2027,
Hata hivyo, UDA kimesema kitachukua hatua ya tahadhari ili kuepuka kudhuru upande wowote.
Bw Omboko Milemba, Katibu Mkuu Msaidizi wa UDA, alisema kuunda muungano ni mazungumzo na makubaliano, na ODM ina haki yake kudai nafasi inayopendelea.
“Kwenye muungano, mambo huletwa mezani. Wakikutana na kuchukua msimamo kama chama cha ODM, hiyo ni sawa — lakini baadaye, tutakutana tutazame mapendekezo yao, wao wataangalia yetu, na tutayalinganisha,” alisema Bw Milemba.
Aliongeza kwamba yale ambayo pande zote zitakubaliana ndiyo yatatumiwa na muungano.
Huku Mbunge wa Emuhaya akionekana kuchukua tahadhari, viongozi wengine wa juu wa UDA wakiwemo Mwenyekiti wa Taifa Cecily Mbarire na Katibu Mratibu Vincent Kawaya, waliepuka kutoa maoni kuhusu suala hilo.
Hata hivyo, kundi la wabunge wa UDA kutoka eneo la Prof Kindiki limekataa madai ya ODM, likimtahadharisha Rais dhidi ya kumtupa wakili huyo kwenye tiketi ya 2027.
“Ujumbe wetu kwa Rais ni wazi, Mlima Kenya Mashariki unasimama naye kikamilifu, lakini uaminifu wetu unaambatana na nafasi ya Kindiki uongozini,” alisema Mbunge wa Buuri, Mugambi Rindikiri.
“Kwa miongo, eneo letu limeunga mkono wengine kupata uongozi wa kitaifa. Sasa, kwa kuwa mmoja wetu anashikilia wadhifa wa juu, hakuna anayepaswa kujaribu kumuondoa. ODM iache kumezea mate hiyo nafasi kwa sababu si ya kugombewa.”
Wakizungumza Jumatatu, wabunge hao,walionya kwamba jaribio lolote la kubadilisha Prof Kindiki litakuwa kifo cha kisiasa kwa Rais.
Walisema ODM inajaribu kulazimisha Ruto kuaichia wadhifa wa naibu rais kama sehemu ya mpangilio mpya wa kugawana madaraka.
“Wenzetu kutoka Eneo la Ziwa lazima waelewe kuwa kiti hiki ni cha Mlima Kenya Mashariki,” alisema Mpuru Aburi. “Tuko tayari kukilinda mwaka wa 2027 na baada yake. Tumekuwa tukisubiri muda mrefu kutambuliwa, na hatutaruhusu fursa hii ipotee.”
Onyo lao linaashiria wasi wasi unaokua ndani ya wandani wa Rais Ruto hasa wa Mlima Kenya Mashariki kutokana na ripoti kwamba ODM inadai wadhifa wa juu katika mpangilio wowote wa muungano wa 2027 na Kenya Kwanza.
Wabunge hao wanasisitiza kuwa wadhifa wa naibu rais hauwezi kujadiliwa.