Mashirika ya Kijamii Pwani yaitaka NCIC imchukulie hatua Rais Ruto kwa kauli tata
MASHIRIKA ya kijamii kutoka Pwani sasa yanaitaka Tume ya Kitaifa ya Uwiano na Utangamano Nchini (NCIC) kumchukulia hatua Rais William Ruto kufuatia matamshi yake ya hivi majuzi kuhusu maandamano yanayoendelea nchini.
Viongozi hao wamesema kauli ya rais ya kuagiza maafisa wa usalama kulenga miguu ya waandamanaji si tu inakiuka katiba, bali pia inachochea ukiukaji wa haki za binadamu.
“Inahuzunisha kuona Rais anatoa matamshi ambayo hayaendani na katiba. Hakuna mtu aliye mkubwa kushinda sheria. Tunataka waitwe na wahukumiwe kwa matendo yao,” alisema Khalifa Khalef wa shirika la Haki Yetu akizungumza Jumapili mjini Mombasa.
Bw Khalef alisema maandamano hayo hayaendeshwi na kabila fulani bali ni Wakenya waliokata tamaa na uongozi wa taifa.
Bw Munira Ali, mwanaharakati wa haki za binadamu, alilaani mauaji yanayoshuhudiwa wakati wa maandamano akisema hali hiyo ni tisho kwa maisha ya raia wasio na hatia.
“Tunaomboleza vifo vya vijana wetu. Serikali ifanye juhudi ya dharura kukomesha unyama huu,” alisema Bi Munira.
Kwa upande wake, Hussein Khalid wa shirika la HAKI Africa alisema kuwa zaidi ya Wakenya 40 walipoteza maisha yao katika maandamano ya Julai 7 kutokana na matumizi ya nguvu kupita kiasi na maafisa wa usalama.
“Wanaoandamana si wahuni wala magaidi. Ni raia wa kawaida wanaodai haki zao. Rais hana mamlaka ya kuagiza watu hao wapigwe risasi,” alisema Bw Khalid.
Aliongeza kuwa haki za kibinadamu haziwezi kutumiwa kama nyenzo ya kisiasa.
“Huwezi kufanyia siasa haki za kibinadamu. Kama mahakama imeondoa hukumu ya kifo, wewe ni nani kuagiza hukumu hiyo kwa waandamanaji?” alihoji.
Yusuf Abubakar, ambaye pia ni mwanaharakati, alitoa wito kwa serikali kuwaachilia vijana waliokamatwa, kuwarejesha waliopotezwa, kulipa fidia kwa familia za waliouawa au kujeruhiwa, na kuwakamata maafisa wote waliohusika na ukatili huo.
“Hatuhitaji mazungumzo. Kinachohitajika ni serikali kulinda haki za binadamu na kutekeleza sheria kwa wote,” alisema.
Viongozi hao pia walimtaka kiongozi wa Azimio Raila Odinga kusimamia utekelezaji wa makubaliano yaliyowekwa kati yake na serikali ili kuwalinda wananchi.