Habari

Mashirika yatishia hatua kali baada ya Wakenya kutekwa nyara Uganda

Na MISHI GONGO October 6th, 2025 Kusoma ni dakika: 3

MASHIRIKA ya kutetea haki za kibinadamu nchini yametishia kutatiza shughuli katika afisi za ubalozi wa Uganda nchini Kenya iwapo Bw Bob Njagi na Nicholas Oyoo, watetezi wa haki za kibinadamu hawataachiliwa ndani ya masaa 24.

Kukamatwa na kuzuiwa kwao kumezua hasira miongoni mwa mashirika ya kijamii na kuzua hofu kuhusu ukandamizaji wa watu ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Bw Njagi na Oyoo, wanasemekana kukamatwa mjini Kampala mapema wiki hii na wanaume wanaoaminika kuwa maafisa wa usalama wa Uganda.

Hadi sasa haijulikani walipo, hali iliyochochea wito wa kuingilia kati mara moja kutoka kwa serikali ya Kenya na mashirika ya haki za binadamu katika Jumuiya Afrika Mashariki.

Akizungumza na wanahabari mjini Mombasa Jumapili, mtetezi wa haki za binadamu Bw Edwin Shamir alitoa wito wa kuachiliwa mara moja kwa wanaharakati hao.

“Tuko hapa kudai kuachiliwa kwa Bob Njagi na Nicholas Oyoo waliotekwa na kuzuiliwa kinyume cha sheria nchini Uganda,” alisema. “Tunatoa wito kwa Rais wa uganda Yoweri Museveni, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Uganda, Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, Wizara ya Mambo ya Nje ya Kenya na Ubalozi wa Kenya mjini Kampala kuchukua hatua za haraka.”

Bw Shamir alitaja tukio hilo kama kitendo cha aibu kilichotekelezwa na serikali ya Uganda, akililaumu taifa hilo kwa kukiuka sheria za kimataifa za haki za binadamu na Mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki unaopiga marufuku kukamatwa kiholela na mateso.

Alisema tukio hilo linaonyesha mtindo unaoendelea wa kunyanyasa wanaharakati katika eneo hilo.

“Hivi karibuni, serikali ya Tanzania ilimteka na kumtesa Boniface Mwangi na Agatha Atuhaire kabla ya kuwatelekeza mpakani mwa nchi zao. Sasa Uganda inarudia makosa hayo hayo dhidi ya wanaharakati wenzetu wa Afrika Mashariki,” alisema.

Katika kikao hicho hicho, Bw Zedekiah Adika, mwenyekiti wa Mtandao wa Mashirika ya haki za binadamu Pwani, alionyesha mshikamano na wanaharakati waliotekwa na kumtaka Rais William Ruto kuingilia kati.

“Hawa ni Wakenya waliotekwa na sasa wako Uganda. Ni jukumu la Rais kutumia mamlaka yake kuhakikisha wako salama na warudishwe nyumbani. Ikiwa kuna tuhuma dhidi yao, wachunguzwe hapa Kenya. Hatuna imani na mfumo wa haki wa Uganda kutokana na jinsi ulivyoshughulikia kesi za kisiasa hapo awali,” alisema.

Bw Walid Sketty alieleza kuwa ukimya kutoka kwa viongozi wa kikanda unatia wasiwasi na kuwalaumu wabunge wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa kutojitokeza kutetea haki za wananchi.

“Watu wanatekwa nchini Tanzania na Uganda, lakini wawakilishi wetu katika Bunge la Afrika Mashariki wako kimya. Lazima wawajibishwe,” alisema.

Bw Francis Auma, afisa wa majibu ya haraka wa shirika la MUHURI, alisema muungano wa mashirika ya haki za binadamu umetoa muda wa saa 24 kwa serikali ya Uganda kuwaachilia Wakenya hao wawili la sivyo watakabiliwa na maandamano makubwa.

“Ikiwa hawataachiliwa, tutasimamisha shughuli zote katika ubalozi na balozi ndogo ya Uganda nchini Kenya. Serikali lazima ilinde raia wake; kushindwa kufanya hivyo hakutapita kimya,” alionya Bw Auma.

Mwanaharakati mwingine, Bi Harriet Mugenda, alihimiza Wizara ya Mambo ya Nje na Diaspora ya Kenya kuchukua hatua rasmi za kidiplomasia kuhakikisha wanaharakati hao wanaachiliwa.

“Mamlaka ya Uganda lazima yaache kulenga wanaharakati wa mataifa mengine na kuheshimu wajibu wao wa kimataifa. Ikiwa hakuna hatua zitakazochukuliwa, tutalipeleka suala hili katika Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki na Tume ya Afrika ya Haki za Binadamu,” alisema.

Wanaharakati hao walisema utekaji huo ni dalili ya kupungua kwa nafasi ya kiraia katika ukanda wa Afrika Mashariki.

“Hatupaswi kuruhusu mwenendo huu wa ukandamizaji kuvuka mipaka bila kupingwa. Utetezi wa haki za binadamu si ugaidi,” alisema Bw Shamir.

Makundi hayo ya kijamii yanaamini ukandamizaji huo unahusiana na uchaguzi mkuu ujao wa Uganda, wakilinganisha hali hiyo na visa vya zamani vya kisiasa nchini humo na Tanzania.

“Kisa cha Njagi na Oyoo ni ukumbusho kuwa serikali zinatumia utekaji kimya kimya kuzima sauti za upinzani. Tunatoa wito kwa viongozi wa Afrika Mashariki kuacha kuwatendea raia kana kwamba ni wanyama wanaowindwa,” alisema Bw Sketty, mwanaharakati mwingine.

Watetezi wa haki wametangaza kuwa wataendelea na kampeni zao hadi Wakenya hao wawili waachiliwe na waliohusika wachukuliwe hatua.

“Hatutakaa kimya wakati wenzetu wanateswa, kufungwa au kupotezwa. Mwaka wa 2025 umekuwa wa majonzi ya kutosha. Tunakataa kuzoea utekaji kama njia ya udhibiti wa kisiasa,” alisema Bw Sketty.

Kufikia wakati wa kuchapisha nakala, serikali za Kenya na Uganda zilikuwa bado hazijatoa taarifa rasmi kuthibitisha kukamatwa au walipo wanaharakati hao.

Mashirika ya haki za binadamu yameapa kuendelea kushinikiza hadi Njagi na Oyoo waachiliwe salama.