Maswali Kuria akijiuzulu baada ya kudai ‘hakutakuwa na uchaguzi 2027’
MSHAURI Mkuu wa Rais William Ruto kuhusu Masuala ya Kiuchumi Moses Kuria amewaacha Wakenya na maswali mengi kwa kujiuzulu siku chache baada ya kudai “hakutakuwa na uchaguzi mkuu 2027”.
Kwenye ujumbe alioandika katika akaunti yake ya mtandao wa kijamii wa X Juni 30, Bw Kuria alitaja ripoti ya Kriegler kuhusu ghasia za uchaguzi mkuu wa 2007 na mvutano kuhusu uteuzi wa makamishna wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka, kama kiashiria kuwa Kenya haitakuwa tayari kwa uchaguzi utakaoaminika 2027.
“Kwa hivyo, wazee wataketi na kuamua ni heri taifa liendelee na uongozi wa sasa ili kuzuia machafuko,” alieleza Bw Kuria, kauli iliyowakera viongozi wa upinzani Kalonzo Musyoka na Rigathi Gachagua walionya kuwa kauli kama hizo zinaweza kuleta taharuki na fujo nchini.
Hata hivyo, Bw Kuria hakufafanua ikiwa kauli yake kuhusu uchaguzi mkuu ilikuwa ya kibinafsi au iliakisi msimamo wa serikali ya Kenya Kwanza.
Lakini wiki mmoja baadaye, mnamo Jumanne, Julai 8, 2025, Bw Kuria alitumia jukwaa hilo hilo la mtandao wa kijamii kuthibitisha kuwa alikutana na Rais Ruto ambaye alikubali kujiuzulu kwake.
“Leo Jumanne jioni nilikutana na bosi wangu na rafiki yangu Rais William Ruto. Rais alikubali, kwa uzuri, uamuzi wangu wa kujiuzulu kutoka serikali,” alieleza Mbunge huyo wa zamani wa Gatundu Kusini.
Jumanne, Bw Kutia alimshukuru Rais Ruto kwa kumpa nafasi ya kuhudumu katika nyadhifa mbalimbali katika serikali yake, akiangazia mchango wake katika Ajenda ya Kuchochea Maendeleo kutoka Mashinani (BETA).
“Namshukuru Rais Ruto kwa nafasi ya kuhudumu kama Waziri wa Uwekezaji, Biashara na Viwanda kwa miezi 11, Waziri wa Utumishi wa Umma kwa miezi tisa, na Mshauri Mkuu wa Masuala ya Kiuchumi kwa miezi 10,” akaandika.
“Nikiondoka kwenda kushughulika na mambo yangu ya kibinafsi, nina fahari kwamba nilifurahia kazi niliyofanya kufanikisha utekelezajiwa ajenda ya maendeleo ya BETA, niliyoshiriki katika kusukwa kwake,” akaongeza.
Muda mfupi baada ya Bw Kuria kujiuzulu mchanganuzi wa masuala ya kiasa Herman Manyora alisema hatua hiyo inaashiria kuwa serikali ya Rais Ruto inaendelea kupoteza umaarufu.
“Hali sio shwari katika serikali ya Ruto. Dalili za mvua ni mawingu……….. wengi wataendelea kujiondoa haswa kuanzia mwanzoni mwa mwaka ujao 2026. Iweje kwamba mshauri wa Rais kuhusu masuala ya kiuchumi anajiondoa wakati ambapo ni masuala yayo hayo ya kiuchumi yanayochochea maandamano ya Gen Z?” akauliza.
Ikulu ya Rais imekimya kuhusu kujiuzulu kwa Bw Kuria ambaye kabla ya kuteuliwa serikalini aliwania ugavana wa Kiambu na kushindwa na Kimani Wamatangi.