Maswali maafisa wa KWS walioshtakiwa kwa kuteka mvuvi Brian Odhiambo wakisalia kazini
MAAFISA sita wa Shirika la Huduma kwa Wanyamapori (KWS) ambao walishtakiwa kuhusiana na kutekwa nyara kwa mvuvi wa Nakuru Brian Odhiambo, bado wanahudumu kwenye nyadhifa zao licha ya kupambana kortini kwa kosa la uhalifu zaidi ya miezi mitatu iliyopita.
Ufichuzi huo ulitokea kortini Jumatatu wakati wa kusikizwa kwa kesi ambapo maafisa hao wa KWS, wanakabiliwa na mashtaka ya utekaji nyara wa mvuvi huyo.
Mkuu wa Mbuga ya Ziwa Nakuru, Bw Emmanuel Koech, alikuwa na wakati mgumu kueleza kwa nini maafisa hao hawajafutwa kazi.
Mawakili wa familia ya Bw Odhiambo na Chama cha Wanasheria Nchini (KWS), walimtaka Bw Koech kuelezea kwa nini maafisa hao wangali wanahudumu katika nyadhifa zao.
Polisi hao ambao walifikishwa kortini mnamo Machi 6, walikanusha mashtaka ya kupanga njama ya kumteka Bw Odhiambo.
Mahakama iliambiwa kisa hicho kilifanyika Januari 18 katika eneo la Kivumbini, viungani mwa jiji la Nakuru.
Bw Koech alithibitisha kuwa polisi hao wanalipwa mishahara kama kawaida wakiyatekeleza majukumu yao.
Hata hivyo, mawakili wa familia ya Bw Odhiambo walizua hoja kuwa kuendelea kwao kuwa kazini kutahitilafiana na uchunguzi ambao unaendelea.
Maafisa hao wa KWS ni afisa wa ngazi ya juu wa cheo cha sajini Francis Wachira, Alexander Lorogoi, Isaac Ochieng’, Michael Wabukala, Evans Kimaiyo na Abdulrahman Suli.
Kifungu cha sita cha Katiba kuhusu uongozi na uwazi kinahitaji afisa yeyote anayeshikilia afisi ya umma na anakabiliwa na mashtaka ya uhalifu, asimamishwe kazi hadi kesi hiyo isikizwe na kuamuliwa.
Bw Koech ambaye alikuwa akitoa ushahidi kwenye kesi hiyo, hata hivyo, alishikilia kuwa maafisa hao wa KWS hawawezi kufutwa hadi wapatikane na hatia.
Akiwa mbele ya Hakimu Mwandamizi, Bw Kipkurui Kibellion, Bw Koech aliambia mahakama kuwa KWS ilikuwa imeanza kuchukua hatua za kinidhamu kupitia asasi zake dhidi ya sita hao.
“Baada ya afisa wa KWS kushtakiwa kortini kuna mchakato ambao shirika lenyewe hufuata kuwaadhibu. Hata hivyo, sita hawa hawajapitishwa kwenye mchakato wote ndio maana hawajafutwa kazi,” akasema Bw Koech.