Maswali mengi polisi 300 wakijaribu kukamata Sudi nyumbani usiku
Na ONYANGO K’ONYANGO
JUHUDI za polisi kumkamata Mbunge wa Kapseret Oscar Sudi nyumbani kwake mnamo Ijumaa usiku zilikosa kutimia hata baada ya kuzingira boma hilo kwa muda wa zaidi ya saa kumi.
Makazi ya Bw Sudi ambaye ni mwandani wa Naibu Rais Dkt William Ruto, pia yalizingirwa na mamia ya vijana wenye hamaki ambao walikuwa tayari kukabiliana na polisi hao waliokuwa wakimwandama mwanasiasa huyo.
Vijana hao waliojihami kwa mikuki na mishale kando na silaha nyingine hatari, walizua kioja walipozingira boma hilo na kuapa kwamba walikuwa tayari kukabiliana na polisi hao.
Kamanda wa polisi wa Kaunti ya Uasin Gishu Johnstone Ipara aliongoza wenzake katika juhudi za kukabiliana na vijana hao ili kufikia boma la mwanasiasa huyo.
Ingawa hivyo, polisi hao walivunja lango na kuingia nyumbani kwa Bw Sudi Jumamosi asubuhi lakini hawakumpata. Hapo awali, umeme ulikatizwa usiku kucha nyumbani kwa Bw Sudi, polisi hao wakimtaka ajisalimishe huku makundi ya vijana nao wakitishia kuwajeruhi kwa mikuki na mishale.
Polisi walilazimika kufyatua risasi hewani mara tano kuwatawanya vijana hao ambao pia walikuwa wakikata miti na kuangusha barabarani huku wakipiga mayowe na hata kuegesha matingatinga na kumwaga ‘milima ya udongo’ kwenye njia ya kuelekea kwa Bw Sudi.
Hata hivyo, Bw Ipara na polisi wenzake walifanikiwa kufika nyumbani kwa Bw Sudi saa tisa na nusu asubuhi ya Jumamosi. Hapo awali alikuwa amewarai vijana hao wawe watulivu wakiwa na matumaini kwamba Bw Sudi angejisalimisha.
Mbunge Mwakilishi wa kike wa Uasin Gishu Gladys Shollei ambaye ni wakili wa Bw Sudi alisema polisi walifanya upekuzi nyumbani mwa Bw Sudi baada ya kuvunja lango kuu la boma lake.
Mmoja wa wakazi alishangaa ni kwa nini zaidi ya maafisa 300 walifika hapo, tena usiku.
“Wana lengo gani kuleta zaidi ya maafisa 300 usiku? Na wathubutu kumkamata na sisi tutakabiliana nao kama wanaume,” akasema.