Habari

Maswali Waititu akiteuliwa kiongozi wa chama

Na MOSES NYAMORI February 4th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

ALIYEKUWA Gavana wa Kiambu Ferdinand Waititu amepata chama cha kisiasa, jambo linalozua maswali kuhusu ufaafu wake kusimamia chama baada ya kuondolewa afisini.

Bw Waititu ameteuliwa kuwa kiongozi mpya wa chama cha Farmers Party ambacho kilikuwa kikiongozwa na aliyekuwa katibu wa wizara Bw Irungu Nyakera, ambaye kwa sasa anahudumu kama mwenyekiti wa bodi ya Jumba la Kimataifa la Mikutano (KICC). Chama hicho cha Farmers Party kilianzishwa na marehemu David Nduati mnamo Mei 2012 na ni chama tanzu cha muungano wa Kenya Kwanza.

Katika notisi iliyochapishwa katika magazeti ya Jumanne, Bw Waititu alitajwa kuwa kiongozi wa Farmers Party kufuatia mkutano wa Kamati Kuu ya Kitaifa ya chama (NEC).

“Taarifa inatolewa kwa umma kwamba kufuatia kikao cha Kamati Kuu ya Taifa (NEC), viongozi wafuatao wa chama waliteuliwa kwa mujibu wa Katiba ya Chama cha Farmers Party,” chama hicho kilisema.

Bw John Wambugu ameteuliwa kuwa Naibu Kiongozi wa Chama (Sera na Mikakati), Bw Nicholas Ikui (Naibu Kiongozi wa Chama – Ukusanyaji wa Rasilimali, Bw Thomas Omboga (Mwenyekiti wa Kitaifa), Bw Stephen Maina (Naibu Mwenyekiti wa Kitaifa – Mipango na Masuala ya Kisiasa), Bw Norman Wambua (Naibu Katibu Mkuu – Masuala ya Kisiasa), na Bi Catherine Ngiabi (Naibu Mweka Hazina wa Kitaifa – Fedha na Ukaguzi) miongoni mwa viongozi wengine wakuu.

Bw Waititu alitimuliwa kama gavana wa Kiambu mwaka wa 2020, na hivyo kuzimwa kushikilia ofisi ya umma isipokuwa aokolewe na mahakama.

Mkuu huyo wa zamani wa kaunti, mnamo Jumanne, alikataa kuzungumzia jukumu lake jipya katika chama, akisema atazungumza ‘kwa wakati ufaao’.

Sura ya Sita ya Katiba kuhusu Uongozi na Uadilifu inaweka wazi kwamba afisa wa serikali aliyefukuzwa kwa sababu ya matumizi mabaya ya ofisi hawezi kushikilia wadhifa wowote wa serikali.

Ingawa chama cha siasa si ofisi ya serikali, kwa kiasi fulani hufadhiliwa na Hazina ya Kitaifa pale kinapokidhi mahitaji ya sheria.

Mtaalamu wa masuala ya Katiba, wakili Bobby Mkangi, hata hivyo, anasema kuwa vyama vya siasa havizingatiwi kama mashirika ya umma licha ya kufadhiliwa.

Alisema hakuna tatizo kwa Bw Waititu kuwa kiongozi wa chama kuwa kuwa uteuzi wake ulifanywa kwa mujibu wa katiba ya chama.