Habari

Matapeli sasa wanalenga wanaotafuta kazi za polisi

Na JOSEPH WANGUI December 20th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

KWA mtazamo wa kwanza ilionekana barua halisi, ikiwa na muhuri wa serikali, nembo ya taifa, hata nambari ya kumbukumbu na maelezo ya jinsi ya kuripoti chuo cha mafunzo ya maafisa wa polisi.

Kwa Peter, mwenye umri wa miaka 23 (jina lake halisi limebanwa), ilikuwa jibu la maombi ya miaka mingi. Familia yake ilisherehekea kimya kimya, majirani wakampongeza, wote wakiamini alikuwa amejiunga na Huduma ya Kitaifa ya Polisi (NPS).

Ndipo ukweli mchungu ukajitokeza kwamba hati hiyo ilikuwa ghushi, udanganyifu uliopangwa kwa ustadi kuiba matumaini na pesa zilizotafutwa kwa jasho. Ndoto ya kazi thabiti ikayeyuka.

Kisa cha Peter ni miongoni mwa makumi ya visa vinavyotikisa nchi. Kote Kenya, walaghai wanawalenga vijana waliokata tamaa kwa kuuza barua bandia za ajira ya polisi kwa hadi Sh700,000 kila moja. Ulaghai huu unaacha familia zikiwa na madeni, aibu na majonzi.

Kwa miezi kadhaa, mchakato wa kuajiri makurutu wa polisi ulikuwa ukitangazwa kwa upana, matangazo yakiambatishwa na maelezo rasmi kusisitiza kuwa ni bure, wazi na wa haki. Hata hivyo, licha ya hakikisho hilo, mtandao wa walaghai umeendelea kuwanasa wanaotafuta kazi kwa kuuza barua bandia na ahadi za “nafasi zilizohakikishwa”.

Wanalenga vijana wanaokabiliwa na ukosefu mkubwa wa ajira na gharama ya juu ya maisha.

Misako ya Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) imefichua ukubwa wa ulaghai huu, huku washukiwa kadhaa waliopata mamilioni ya shilingi kutoka kwa waathiriwa wasiokuwa na habari wakikamatwa.

Uchunguzi unaonyesha mtandao uliopangwa vyema. Walaghai huuza barua bandia kwa kati ya Sh300,000 na Sh700,000 kwa mtu mmoja. Kila moja huishia kwa maumivu waathiriwa wanapofika vituo vya mafunzo na kuambiwa hawakubaliki.

Katika operesheni moja wikendi iliyopita, makachero kaunti ya Nairobi waliwakamata washukiwa wanne waliodaiwa kuwatapeli vijana 11 jumla ya Sh6.4 milioni. Kumi walikuwa wamelipa kati ya Sh600,000 na Sh700,000 kila mmoja, huku mmoja akitoa Sh450,000 akiamini amepata nafasi katika Chuo cha Mafunzo ya Polisi cha Kiganjo. Polisi walipata Sh700,000 taslimu na barua 10 bandia kwenye gari la mshukiwa.

DCI ilisema kwamba washukiwa waliwalenga waliokosa kufaulu wakati wa zoezi la hivi karibuni la uajiri, lililogubikwa na mvutano wa kisheria kati ya Inspekta Jenerali wa Polisi na Tume ya Huduma ya Polisi.

Msako huu ulikuwa miongoni mwa misako kadhaa. Mwezi uliopita, makachero wa Kilimani walimkamata mshukiwa aliyedaiwa kulaghai familia saba Sh2.5 milioni kwa kisingizio cha ajira ya polisi. Alijifanya “broka” mwenye uwezo wa kupata kazi, akitoa nyaraka bandia. Licha ya kukanusha mashtaka na kuachiliwa kwa dhamana ya Sh1 milioni, polisi walipata barua kadhaa bandia.

Katika kisa kingine Kilimani, mshukiwa alikamatwa baada ya kuwalaghai wanaotafuta kazi Sh2.5 milioni kwa ahadi za nafasi zilizohakikishwa. Polisi walipata barua 20 bandia. Katikati ya jiji la Nairobi, wanawake wawili walikamatwa kwa kutumia barua bandia, polisi walipata Sh330,200 zinazodaiwa kuwa mapato ya ulaghai.

Mtindo huu unajirudia: kila NPS inapotangaza uajiri wa makurutu, walaghai hujitokeza wakiahidi nafasi kwa malipo. Mara nyingi, waathiriwa huwa ni familia zinazouza mifugo, kukopa kwa riba kubwa au hutumia akiba yote ambao huachwa na fedheha na hasara. Wengi hawaripoti kutapeliwa kwa aibu.

NPS imejaribu kukabiliana na ulaghai kwa kampeni za uhamasishaji, ikisisitiza kuwa ajira si ya kununua. Hata hivyo, walaghai hutumia tamaa ya wanaosaka kazi kuwapotosha na kulaghai baadhi ya watu.