Mateso, vilio katika kaunti
Na WAANDISHI WETU
MZOZO kati ya Bunge la Taifa na lile la Seneti kuhusu mgao wa pesa za kaunti umesababisha mahangaiko na mateso tele kwa maelfu ya wafanyikazi katika zaidi ya kaunti 30.
Bunge la Taifa liliidhinisha Sh316 bilioni ilhali Baraza la Magavana na Seneti zinasisitiza zipewe Sh335 bilioni, ambazo hata Rais Uhuru Kenyatta alisema hazipo.
Tukienda mitamboni, ni chini ya kaunti 17 zilizokuwa zimewalipa wafanyikazi mshahara wa Julai, jambo ambalo limelazimu chama cha Wafanyikazi hao (KCGWU) kutishia kuanza mgomo Jumanne, iwapo hawatakuwa wamelipwa kufikia kesho Jumatatu.
Hata hivyo, Jumatatu ni Sikukuu na huenda malipo hayo yasifanyike.
Mashinani, wafanyikazi walielezea masaibu wanayopitia, wengi wakiwa wanawatoroka wenye nyumba.
Katibu wa Muungano wa Wafanyakazi wa Umma tawi la Tharaka Nithi, Bw Festus Nyaga Gaicu alisema Jumamosi kwamba wanajiandaa na mgomo.
“Subira yetu imeisha kabisa na ifikapo Jumanne hatutakuwa na hiari ila kufuata agizo la afisi yetu ya kitaifa na kuandamana barabarani kudai mshahara,” akasema Nyaga Gaicu.
Mfanyikazi katika kaunti hiyo ya Tharaka Nithi ambaye hakutaka kutajwa, alisema wamelazimika kukopa pesa kupitia simu.
“Wengi wetu tumechukua mikopo na tunategemea kiasi kidogo cha hela tunachopata kila mwisho wa mwezi ili kujikimu na sasa ni balaa tupu,” alisema.
Katika kaunti ya Meru, Antony Mwiti alisimulia jinsi ambavyo familia yake imo hatarini, na kwamba anaomba Mungu wasiugue.
“Hatujapata mshahara wa Julai na tunapitia changamoto kuu kwa sababu hatuwezi kununua chochote,” akasema.
Katika kaunti ya Embu, wafanyikazi wa kaunti wanaishi kwa hofu ya kufukuzwa kutoka kwa nyumba walizopangisha.
“Malandilodi wamekuwa wakitishia kutufurusha kutoka nyumba tulizokodisha kwa sababu hatujawalipa. Pia tunahitaji pesa za kununulia familia zetu chakula,” alisema Bi Patricia Wanja.
“Tumegeuzwa watu wa kuwatoroka landilodi kwa kuwa hupata pesa zake tarehe ya kwanza ya mwezi na sasa imekuwa siku tisa, utafanya nini?”aliuliza mfanyikazi mwingine.
Malimbikizi ya madeni
Mwenzake katika Kaunti ya Kirinyaga, Bw Stephen Chege anasema wengi wanajilimbikizia madeni kutoka kwa wakopeshaji wa kibinafsi, japo hawana uhakika watalipwa lini.
“Hali hii ni ya dharura, baadhi yetu wenye mikopo tumezidiwa kwa sababu tunawageukia mashailoki ili kujikimu. Hatuna hata nauli kwa sababu hatujapokea mishahara kwa miezi miwili,” akasema.
“Nilikuwa nimejiahidi kwamba sitawahi kamwe kutumia vifaa ya mikopo kielektroniki lakini sasa nimejipata nikivihitaji kwa sababu sina chakula na watoto wangu wanahitaji kusafiri kwa likizo,” alisema mfanyakazi mwingine katika Kaunti ya Murang’a.
Jaji Mkuu David Maraga alishauri pande husika zijadiliane na kupata muafaka.
Ripoti za Alex Njeru, Ndungu Gachane, Elijah Mwangi na George Munene