Matiang’i atetea Uhuru kuhusu njama za kusambaratisha ODM
MGOMBEA urais wa Chama cha Jubilee katika Uchaguzi Mkuu wa 2027, Dkt Fred Matiang’i, amemtetea Rais mstaafu Uhuru Kenyatta dhidi ya wanaomshambulia kufuatia kauli zake za hivi majuzi.
Akizungumza jijini Nairobi Jumanne baada ya kuongoza kikao cha kwanza cha chama hicho mwaka huu, Dkt Matiang’i alisema inatia wasiwasi kuona maafisa wa serikali wakikerwa kila mara Rais mstaafu anapopewa nafasi ya kuzungumza, hali inayozua maswali kuhusu sababu ya kelele kuibuka kila Bw Kenyatta anapotoa maoni yake.
Dkt Matiang’i ambaye alikuwa waziri chini ya utawala wa Kenyatta alisema kuwa kukabidhi mamlaka kwa mrithi wake na kustaafu hakumzuii Bw Kenyatta kushiriki au kutoa maoni kuhusu masuala yanayohusu nchi.
“Kiongozi wetu wa chama, licha ya kuwa Rais mstaafu, ana haki ya kushiriki na kujihusisha na masuala ya taifa. Tunawaomba wenzetu katika uongozi wa kitaifa waache kumshambulia kiongozi wetu na kumvuta katika mambo yasiyo na umuhimu. Wana kazi nyingi za kufanya,” alisema Dkt Matiang’i.
Alidai kuwa uwepo wa kiongozi wa Jubilee unaonekana kuwakasirisha baadhi ya watu, wakiwemo walio serikalini.
Wakati huo huo, Dkt Matiang’i alikanusha madai kuwa Jubilee inahusika katika njama za kugawanya chama cha ODM kwa lengo la kuimarisha muungano wake kuelekea uchaguzi wa 2027.
Badala yake, alisema Jubilee inaamini katika misingi ya kidemokrasia inayapatia vyama vingine nafasi ya kustawi bila kuingiliwa.
“Sisi ni chama cha amani. Tunatakia vyama vingine vyote vya kisiasa heri tunapoendelea mbele. Hatuko kwenye mgogoro na yeyote na hatutaki migogoro. Tunaamini kwa dhati katika demokrasia ya vyama vingi,” alisema.
Aliongeza kuwa ingawa vyama mbalimbali vinafanya mazungumzo ya kuunda miungano, Bw Kenyatta hajahusika kwa namna yoyote katika juhudi zozote za kuvuruga ODM kama inavyodaiwa na baadhi ya viongozi wa serikali jumuishi.
Katibu Mkuu wa Jubilee, Bw Jeremiah Kioni, pia alikanusha madai ya matumizi mabaya ya fedha zilizotengewa maajenti wa Azimio katika uchaguzi wa 2022, akiyataja kuwa tuhuma zisizo na msingi zinazolenga kupotosha umma.
Bw Kioni alisema madai hayo, yaliyotolewa na Mbunge wa Suna Mashariki Junet Mohamed, yalipaswa kushughulikiwa mapema na uongozi wa Azimio.
Aidha, Bw Kioni alidai kuwa kama fedha hizo zingesimamiwa ipasavyo, marehemu Waziri Mkuu Raila Odinga angeibuka mshindi wa urais.
Chama cha Jubilee pia kilisema kimeweka mikakati madhubuti ya kuimarisha ngome zake kote nchini kikijiandaa kwa uchaguzi wa 2027.