Habari

Matiang'i awataka viongozi wa kidini kuisaidia serikali kufanikisha vita dhidi ya mihadarati

October 8th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na CECIL ODONGO

WAZIRI wa Usalama wa Ndani Dkt Fred Matiang’i amefichua kwamba uchunguzi unaendelea dhidi ya watu 30 maarufu wanaoshukiwa kushiriki biashara ya uuzaji wa mihadarati katika eneo la Pwani.

Dkt Matiang’i amesisitiza Jumatatu kwamba ziara yake majuzi katika mtaa wa Kisauni, jijini Mombasa ilimpa picha halisi ya namna wakazi wametekwa na uraibu wa kutumia mihadarati, akisema watu mashuhuri wanaoshiriki ulanguzi wa dawa za kulevya ndio wa kulaumiwa kwa hilo.

“Tuna kesi 30 za watu mashuhuri wanaotoka Pwani ambao wanashiriki biashara chafu ya uuzaji wa mihadarati. Uchunguzi bado unaendelea na kikosi chetu kiko tayari kuhakikisha wanakabiliwa kisheria,” akasema Dkt Matiang’i.

Akaongeza: “Watu wanaofanya biashara hii si watu wa kawaida. Ni watu wenye hadhi ambao wanaelewa namna ya kusambaza mihadarati hizo.”

Waziri huyo amekuwa akihutubu baada ya kutembelea msikiti wa Jamia jijini Nairobi ambapo ametoa wito kwa viongozi Waislamu washirikiane naye kufanikisha vita dhidi ya mihadarati.

Aidha amewahakikishia Waislamu kwamba serikali haihusiki kamwe na visa vya kuuawa kwa watu wanaokamatwa akiahidi kuchunguza visa hivyo na kuwachukulia hatua kali maafisa wa polisi watakaopatikana kuhusika.

“Hakuna sera ya serikali inayopigania upato mauaji ya raia. Hili ni suala ambalo sasa tumemakinikia kwa sababu haiwezekani kwamba mtu anakamatwa kisha anapotea katika hali isiyoeleweka. Kuna mwongozo wa kisheria wa kuwaadhibu wahalifu,” akasema.

Viongozi wa Waislamu waliohutubu wameomba serikali kuinua hadhi ya Chuo Kikuu cha Umma na kukipa cheti kama vyuo vingine; jambo ambalo Dkt Matiang’i ameridhia na kuahidi kwamba hilo litatimizwa kabla ya kukamilka kwa mwezi huu wa Oktoba.

Vilevile ametangaza kwamba serikali itafungua ofisi za uhamiaji na usajili mjini Garissa ili kuwazuia Waislamu kukongamano katika afisi zilizoko Nairobi kila mwaka wanaposafiri hadi Saudi Arabia kwa hija.

Kiongozi wa wengi katika Bunge la Kitaifa, Aden Duale naye amewaomba viongozi kutoka maeneo wanakoishi Waislamu wengi washirikiane na serikali kuhakikisha usalama unadumishwa wakati wote.

“Viongozi kutoka ngome za Waislamu lazima washirikiane na serikali kuhakikisha usalama unadumishwa wakati wote. Lazima pia tupige vita dhidi ya mihadarati na mafunzo dini yenye itikadi kali,” akasema Bw Duale.

Mkuu wa Mashtaka ya Umma(DPP) Noordin Haji, Seneta wa Garissa Yusuf Haji, Chansela wa Chuo Kikuu cha Umma Abbas Gullet na viongozi wa Msikiti wa Jamia pia wamehudhuria hafla hiyo.