Habari

Matiang’i roho juu akianza kusaka uungwaji Mlima Kenya

Na DAVID MUCHUI August 18th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

ALIYEKUWA Waziri wa Usalama wa Ndani Dkt Fred Matiang’i sasa analenga kutumia Jubilee na PNU kutanua mawanda yake Mlima Kenya kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027.

Dkt Matiang’i alianza kampeni yake kwenye ukanda huo kwa kuhutubia mkutano wa kisiasa eneo la Timau, Kaunti ya Meru.

Kiongozi wa PNU Peter Munya ndiye alikuwa mwenyeji wake.

Mkutano huo ulihudhuriwa na wanasiasa na viongozi wa nyanjani na Dkt Matiangí akapata muda wa kuwahutubia wakazi moja kwa moja.

Katika mkutano huo, Dkt Matiangí pia alipokea uungwaji mkono kutoka kwa vyama vya kisiasa ikiwepo PDP, KSC na UPA kati ya vyama vingine.

Akiongea katika mkutano huo, Dkt Matiang’i alililia Mlima Kenya umuunge mkono akisema alikuwa mchapakazi alipohudumu kwenye wizara mbalimbali chini ya utawala wa Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta.

“Nilikuwa nimepanga kuzuru Mlima Kenya mnamo Julai lakini nikafutilia mbali ziara yangu kutokana na tukio la kusikitisha mnamo Julai 7. Pia kulikuwa na mipango ya wakora kuingizwa na kuvuruga mikutano yetu. Sasa nitakita kambi hapa na niongee na watu moja kwa moja,” akasema.

Dkt Matiangí alisema kuwa kama vinara wa Upinzani Rigathi Gachagua, Kalonzo Musyoka, Martha Karua na Eugene Wamalwa, wako tayari kushirikiana kuelekea uchaguzi mkuu.

“Tutakubaliana nani atakuwa mpeperushaji bendera wetu lakini kilicho wazi ni kwamba katika uchaguzi mkuu ujao, Wakenya ndio wataamua na wameonyesha wanatuunga mkono. Wakenya hawatachagui viongozi tena kwa kuzingatia kabila,” akaongeza Dkt Matiangí.

Alifunguka na kusema kuwa anaendelea kuongea na viongozi mbalimbali wa kisiasa na lengo lao kuu litakuwa kuwaunganisha Wakenya.

Dkt Matiangí amekuwa akihusishwa na Jubilee yake Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta pamoja na UPA ambayo inaongozwa na Gavana wa Nyamira Amos Nyaribo.

Waziri huyo wa zamani pia alipinga kubinafsishwa kwa Kampuni ya Mafuta ya Kenya Pipeline akisema mchakato sahihi haukufuatwa.

Kiongozi wa PNU Peter Munya alisema kuwa chama hicho kinamuunga mkono Dkt Matiangí kutokana na rekodi yake ya maendeleo na utumishi wake wa kupigiwa mfano kwenye sekta ya umma.

Alidai kuwa utawala wa sasa umevuruga sekta muhimu na inasikitisha sasa viongozi wanatumia pesa za umma vibaya kushiriki mikutano wanayosema ni ya kuinua akina mama.

“PNU na Jubilee zimekubali kumuunga mkono Dkt Matiangí kwa sababu lazima turejeshe nchi hii kwenye mkondo wa utawala wa kuridhisha,” akasema Bw Munya.

Dkt Matiang’i aliandamana na aliyekuwa Waziri wa Elimu Ezekiel Machogu, Katibu Mkuu wa Jubilee Jeremiah Kioni, Seneta wa Kisii Richard Onyonka, Kiongozi wa PDP Omingo Magara na viongozi wengine.

Mkutano huo ulioandaliwa Ntimau unaashiria kuanza rasmi kwa mikutano ambapo Dkt Matiangí atakuwa akikutana na wafuasi wake ambapo atakuwa akilenga kura za Mlima Kenya.