Matokeo ya uchaguzi kuongoza wahudumu wa tuktuk Githurai yafutiliwa mbali
Na SAMMY WAWERU
MATOKEO ya uchaguzi wa viongozi wa muungano wa wahudumu wa tuktuk na magari madogo ya usafiri na uchukuzi Githurai 45, GTMA yamefutiliwa mbali.
Uchaguzi wa mwaka huu, 2020, na uliofanyika Novemba 13, matokeo yaliyotangazwa yalipingwa na baadhi ya wawaniaji, kwa kile walitaja kama shughuli ya upigaji kura na kuzihesabu kukumbwa na utapeli.
Kiti cha mwenyekiti na karani, ni kati ya nyadhifa ambazo wagombea walieleza kutokuwa na imani na matokeo.
Aidha, waliwasilisha malalamishi katika afisi ya Masuala ya Jinsia, Utamaduni na Huduma za Kijamii (SCDO), Kaunti ndogo ya Ruiru, ambayo ilisimamia zoezi hilo lililofanyika katika ukumbi wa mikutano ofisi ya D.O Githurai, chini ya ulinzi wa maafisa wa polisi.
Kwenye mkutano ulioandaliwa jana Alhamisi, kamati ya muda iliyobuniwa na wamiliki wa tuktuk, ilitangaza kuwa afisi ya SCDO imeharamisha matokeo ya uchaguzi huo, baada ya kupata ushahidi wa kutosha kutoka kwa walalamishi ulioonyesha “kulikuwa na utapeli katika shughuli hiyo”.
Kaimu mwenyekiti, Simon Wachira pia alitangaza kwamba imeafikiwa Katiba ya GTMA ifanyiwe marekebisho kabla ya uchaguzi mwingine kuandaliwa.
“Matokeo ya uchaguzi uliofanyika Novemba 13, 2020 yamefutiliwa mbali, baada ya SCDO kuridhishwa na malalamishi yaliyowasilishwa,” Bw Wachira akasema, akirejelea barua ya SCDO.
Kabla uchaguzi mwingine kufanyika, wamiliki wa GTMA wameafikiana kufanyia Katiba ya Muungano huo marekebisho.
Vilevile, wamependekeza viongozi ambao wamekuwa afisini awamu iliyokamilika na awamu za awali wasiwanie nyadhifa za uongozi tena, wakihoji “hakuna maendeleo yoyote waliyotuletea”.
Kwenye mkutano wa jana, Bw Peter Kinyua (mwenyekiti anayeondoka) alitakiwa kuiandikia SCDO barua kusimamisha maandalizi ya uchaguzi mwingine, ili kuruhusu marekebisho ya Katiba kutekelezwa.
SCDO pia imeagiza GTMA kuandaa rejista ya wapigakura ili kuepuka zogo sawa na lililoibuka, wamiliki wakisisitiza kuwa madereva ambao hawana magari hawapaswi kushiriki upigaji kura.
Muungano huo una zaidi ya tuktuk na magari madogo ya usafiri na uchukuzi ndio maruti, 300.