MAUAJI YA MTANGAZAJI: Mwanamume mwenye umri wa miaka 23 azuiliwa kwa siku kadhaa
Na RICHARD MUNGUTI
MWANAMUME mwenye umri wa miaka 23 alifikishwa katika mahakama ya Milimani, Nairobi kwa madai alimuua mtangazaji wa kituo cha redio cha Pamoja FM kinachopeperusha matangazo kutoka mtaani Kibra, Nairobi.
Luqman Mohammed Ibrahim, mahakama iliagiza azuiliwe katika kituo cha polisi cha Kilimani kusaidia polisi kuwatia nguvuni washukiwa wengine sita waliomshambulia Mohamned Hassan Marjan.
Akiwasilisha onbi la kuzuiliwa kwa Luqman afisa wa polisi Paul Mwachiro alimweleza hakimu mkazi Carolyne Muthoni Nzibe kuwa mshukiwa alitiwa nguvuni Jumatatu na mahojiano yanaendelea.
Mwachiro alisema mshukiwa huyu anatazamiwa kuwasaidia polisi kuwasaka washukiwa wengine alioshirikiana nao kutekeleza uhalifu huo wakiwa wamejihami kwa silaha hatari.
Hakimu alifahanishwa mshukiwa anahitajika kupimwa akili ibainike ikiwa akili yake ni timamu kabla ya kufunguliwa mashtaka.
Bi Nzibo aliombwa aamuru mshukiwa azuiliwe siku 14.
Mahakama iliambiwa Marjan aliyekuwa na umri wa miaka 62 alishambuliwa na kundi la wanaume saba waliokutana naye katika eneo la Olimpiks akitoka kazini na kumshambulia.
Aliaga dunia baada ya muda mfupi.
Luqman atarudishwa tena mahakamani Mei 22, 2020, kwa maagizo zaidi.