Habari

Mshukiwa mkuu katika mauaji ya Mwingereza Campbell Scott hatimaye ashtakiwa

Na RICHARD MUNGUTI May 28th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

MSHUKIWA mkuu katika mauaji ya raia wa Uingereza Campbell Scott alishtakiwa Jumanne katika Mahakama kuu ya Makadara.

Alex Mutua alikana mbele ya Jaji James Wakiaga kwamba alimuua Scott usiku wa Februari 16, 2025, katika mtaa wa Pipeline Nairobi.

Mutua aliyejibu shtaka kupitia mtandao amekuwa kizuizini kwa miezi miezi minne.

Mshtakiwa aliomba aachiliwe kwa dhamana.

Ombi hili lilipingwa vikali na upande wa mashtaka.

Kiongozi wa mashtaka aliomba muda wa siku 21 kuwasilisha hati kiapo akisimulia sababu za kupinga Mutua akiachiliwa kwa dhamana.

Mwili wa Scott ulipatikana ukioza katika msitu wa Makongo ulioko kaunti ya Makueni.

Mshtakiwa huyo alirudishwa gerezani hadi Juni 17, 2025 kesi itakapotajwa kwa maagizo zaidi.

Jaji Wakiaga aliamuru idara ya urekebishaji tabia imhoji mshtakiwa pamoja na familia ya mwathiriwa na ripoti hiyo kuwasilishwa kortini kabla ya uamuzi wa dhamana kutolewa.

Mshukiwa mwingine katika mauaji hayo Samuel Musembi Kamitu alijitoa uhai kabla ya kukamatwa na polisi mtaani Dandora Nairobi.

Washukiwa wengine waliotoroka na wanasakwa na polisi ni pamoja na Alphonse Munyao Kilewa almaarufu Edu na Bernard Mbunga Mbusu.

Mutua alikamatwa pamoja na Albunus Mutinda Nzioki aliyeachiliwa na kufanywa shahidi mkuu.