MAUAJI YA SOLEIMANI: Iran yataka Trump akamatwe
CHARLES WASONGA na MASHIRIKA
IRAN imetoa ilani ya kukamatwa kwa Rais wa Amerika Donald Trump na watu wengine 35 kuhusiana na mauaji ya Jenerali Qasem Soleimani Januari 3, 2020.
Mkurugenzi wa mashataka wa Iran Ali Alqasimehr Jumatatu ameomba usaidizi wa polisi wa kimataifa (Interpol) kuiwezesha kumkamata Trump, kulingana na shirika la habari la Fars News.
Amerika inadaiwa kumuua Soleimani, ambaye alikuwa kiongozi wa Kikosi cha Revolutionary Guards katika jeshi la Iran kwa jina, Quds Force.
Aliuawa katika shambulio lililotekelezwa na droni nchini Iraq.
Amerika ilikuwa ikimtuhumu Soleimani kwa kupanga mashambulio dhidi ya wanajeshi wa Amerika nchini Iraq.
Ilidai kuwa jenerali huyo ndiye alipanga mashambulio hayo yaliyotekelezwa na wapiganaji waliokuwa wakisaidiwa na Iran.
Alqasimehr alisema Iran inamtuhumu Trump kwa makosa ya mauaji na vitendo vya kigaidi.
Alisema afisi yake imeiomba Interpol kusaidia katika kukamatwa kwa kiongozi huyo wa Amerika na maafisa wengine wa jeshi la nchini na raia fulani wa Amerika ambao hakutoa majina yao.
“Iran itafuatilia kesi hiyo hata baada ya kukamilika kwa hatamu ya Trump afisini,” kiongozi huyo wa mashtaka akasema.
Nusra mauaji ya Soleimani yasababishe vita kati ya Amerika na Iran.
Hii ni baada ya Iran kushambulia vituo vya Amerika nchini Iraq kwa makombora siku kadhaa baada ya mauaji hayo.