Mawakili waapa kumkabili Joho
Na WINNIE ATIENO
GAVANA wa Mombasa Hassan Joho amepata pigo baada ya Chama cha Mawakili Kenya (LSK) kuapa kusimamisha mpango wa Kaunti ya Mombasa kuongeza ada za leseni za biashara na uegeshaji magari.
Hii ni baada ya serikali ya Kaunti ya Mombasa kuongeza ada za leseni kwa asilimia 100 katika bajeti ya mwaka wa fedha wa 2019/2020.
Wafanyibiashara na wawekezaji katika kaunti hiyo wamekuwa wakilalamika kuhusu ada hizo wakimtaka Bw Joho afanye kikao cha dharura na wadau wote kujadili suala hilo.
Mwenyekiti wa LSK tawi la Mombasa Mathew Nyambena, alisema hatua ya kuongeza ada za leseni ni jambo linalohitaji kusuluhishwa kwa dharura.
“Tumesukumwa sana mpaka tukaamua kuwasilisha kesi mahakamani ili wawekezaji wasiathirike. Sote tunajua kuwa gharama ya kufanya biashara imekuwa ngumu sana kwa kuwa uchumi wa Mombasa umedorora, na basi kuongeza ada hizo ni hujuma,” akasema Bw Nyabena.
Alisema uongozi wa Mombasa unafaa kuweka mazingira bora ya kuvutia wafanyabiashara wala sio kuwavunja moyo.
Kwenye mabadiliko hayo, vilabu vya starehe vimeongezwa ada hadi Sh200,000 kutoka Sh100,000 kwa leseni ya kuuza pombe huku kasino zikitozwa kati ya Sh100,000 hadi nusu milioni kwa mwaka.
Ada ya kuegesha magari imeongezwa kwa asilimia kutoka Sh100 hadi Sh200.
Wiki mbili zilizopita, serikali ya kaunti hiyo iliitisha mkutano wa dharura na wafanyabiashara waliotishia kuhama jiji hilo kama ada hizo hazitapunguzwa.
Hata hivyo, Karani Mkuu wa Mombasa Denis Muganga aliwaahidi kuwa malalamishi yao yatazikiswa.
“Tumesikia malalamishi yenu. Hivyo basi tunawaalika kwa mkutano kujadili suala hili ili tuafikiane,” alisema Bw Muganga.
Wafanyabiashara hao wakiongozwa na mkurugenzi mkuu wa muungano wa wafanyikazi wa hoteli, Sam Ikwaye walimtaka Gavana Joho kufutilia mbali ada hizo mara moja.
“Sheria ya mwaka wa fedha wa 2019/2020 ya Kaunti ya Mombasa inalenga kumnyanyasa na kumdhulumu mfanyibiashara. Kwa nini tunaumizwa ilhali tumewekeza na kubuni nafasi za kazi?” alisema Dkt Ikwaye.
“Kuongeza ada wakati uchumi umedorora ni njia moja ya kumaliza biashara na hatimaye wananchi waanze kuteseka. Ni sharti kaunti iwavutie wawekezaji ili vijana wetu wapate ajira,” akaongeza.
Mfanyabiashara wa mikahawa Bi Patricia Njeri, alishtumu serikali ya kaunti kwa kushindwa kuweka misingi bora na mazingira ya biashara ilhali inaongeza ada hizo.