Mawaziri wapewa likizo ya Krismasi na Mwaka Mpya
Na CHARLES WASONGA
MAWAZIRI wataenda likizo kuanzia Desemba 22, 2020, hadi Januari 3, 2021.
Mkuu wa Utumishi wa Umma Joseph Kinyua amesema Jumamosi kwamba wakati wa likizo, mawaziri hao hawatakuwa wakihudhuria mikutano ya kila wiki ili wawe na nafasi ya kujumuika na familia zao.
“Wakati wa likizo, shughuli za Rais zilizopangwa zitaendelea kama kawaida sawa na kalenda ya Baraza la Kitaifa la Usalama (NSC) na Baraza la Kitaifa la Ushauri kuhusu Usalama (NSAC),” Kinyua akasema kwenye taarifa kwa vyombo vya habari.
Alisema kuwa baraza la mawaziri na kamati zake hazitafanya mikutano isipokuwa endapo Rais atatoa agizo kwamba mikutano ifanyike kujadili jambo la dharura, matukio ya kitaifa yanayoweza kujiri bila kupangwa na yawe na umuhimu mkubwa au haja yoyote ibuka.
Hata hivyo, Bw Kinyua pia amesema wanachama wa Baraza la Kitaifa la Kushughulikia Mikakati ya Kupambana na Covid-19 (NERC) hawataenda likizo. Hii ina maana kuwa Waziri wa Afya Mutahi Kagwe ambaye ni mwenyekiti wa kamati hiyo hataenda likizo.
Mkuu huyo wa utumishi wa umma amefafanua kuwa shughuli nyinginezo za serikali zitaendelea kama kawaida na katika viwango stahiki.