Mazishi bila maiti wala jeneza kwa aliyetekwa nyara Uasin Gishu
FAMILIA moja katika kijiji cha Kabongwa, Kaunti ya Uasin Gishu iliwashangaza wengi ilipoandaa mazishi ya jamaa wao bila uwepo wa jeneza wala mwili.
Edward Kipchumba Terer, ambaye ni mhudumu wa maabara hospitalini, alitoweka mwezi mmoja na nusu uliopita katika eneo lenye utovu wa usalama la Bonde la Kerio, na tangu wakati huo hajapatikana.
Baada ya kushawishika kuwa aliuawa na majangili, familia yake iliamua kuandaa mazishi ya mwigo kwa ajili ya kumkumbuka.
Hii ndio maana wakati wa mazishi hayo picha yake na mali yake chache yaliwekwa parawanja ili wanakijiji waone sura yake kamili huku wakiuliza maswali kuhusu kitendawili cha kukithi kwa mauaji ya kiholela, Bonde la Kerio.
Hafla hiyo iliongozwa na wazee wa jamii waliofanya matambiko ya kutuliza roho ya Terer.
Baba huyo wa watato watano alitoweka mahali pake pa kazi, Kliniki ya Samabalat iliyoko Kaunti-ndogo ya Marakwet Mashariki.
Mhudumu huyo wa afya aliripotiwa kutekwa nyara na watu walioaminika kuwa maafisa wa usalama mnamo Juni 2, mwaka huu, na hajaonekana tangu siku hiyo.
Baadhi ya “waombolezaji” waliangua kilio wakikumbuka siku ambazo walimwona mara ya mwisho na kuyeyuka kwa matumaini yao ya kupata hata mabaki ya maiti yake.
“Ni uchungu kuandaa sherehe ya mazishi ya mtu ambaye mwili wake haujapatikana. Lakini tusipofanya hivyo, moyo wake hautapumzika pema. Ataendelea kutuletea ndoto za kutatiza,” akasema Augustin Limo, ndugu mdogo wa Terer.
Kinyume na mazishi ya kawaida, hakukuwa na ratiba maalum wakati wa “mazishi” hayo.
Baadhi ya waliohudhuria hafla hiyo waliondoka kwa huzuni baada ya shughuli hiyo iliyodumu kwa muda usiozidi saa moja.
Wengine waliamua kusalia nyuma kuiliwaza familia ya Bw Terer.
“Tunaamini kuwa ndugu yetu aliuawa. Nimetafuta kila mahali na tunaambiwa mwili wake haujapatikana,” akaongeza Bw Limo.
Bw Terer alikuwa amehudumu katika kliniki hiyo ya kibinafsi kwa miaka 11.
“Tuliwasilisha ripoti kwa Kituo cha Polisi cha Tot na afisa msimamizi aliahidi kutupasha habari kuhusu hatua ya uchunguzi lakini hajafanya hivyo hadi sasa. Hii ndiyo maana tumeamua kumwandalia mazishi ya mwigo,” akasema Bw Limo.
Kulingana na familia, watekaji nyara waliondoka na simu ya Bw Terer, na hivyo ikawa vigumu kutafuta.
Hata hivyo, Kamanda wa Polisi Kaunti ya Elgeyo Marakwet Peter Mulinde alikana kuwa na ufahamu wowote kuhusu kisa hicho.
“Hatujapokea ripoti rasmi kuhusu kutoweka kwa mtaalamu wa maabara kando na yale tumesoma kwenye mitandao ya kijamii,” Bw Mulinge akaambia Taifa Leo.
Visa vya watu kutoweka kiajabu na mauaji ya kiholela katika Bonde la Keria vimeshamiri ikiwa ni pamoja na mauaji ya Padre mmoja wa Kanisa Katoliki.
Hamna aliyekamatwa kuhusiana na mauaji ya kiongozi huyo wa kidini kwa jina, Allois Cheruiyot Bett.
Mamlaka ya Kuchunguza Utendakazi wa Polisi (IPOA) imekuwa ikiendesha uchunguzi kuhusu kutoweka kwa Bw Terer na haijatoa ripoti mpaka sasa.
“Ipoa ilipokea ripoti kuhusu madai ya kubakwa kwa mhudumu huyo wa afya mnamo Juni 10. Inaendelea na uchunguzi kubaini ikiwa polisi walihusika,” akasema afisa wa mawasiliano wa mamlaka hiyo Dennis Oketch.
Taharuki ilitanda katika Bonde la Kerio mwezi jana pale miili miwili iliyopatikana kando mwa barabara Nakuru ilitambuliwa kuwa ya wakazi wa Tot, kaunti ya Elgeyo Marakwet.