HabariSiasa

Mbinu alizotumia Moi kuzima Mlima Kenya

February 9th, 2020 Kusoma ni dakika: 3

Na WANDERI KAMAU

MIGAWANYIKO ya kisiasa miongoni mwa wanasiasa wa eneo la Mlima Kenya, imetajwa kuwa sababu kuu iliyompa mwanya Rais Mstaafu Daniel Moi kulitenga eneo hilo kisiasa kwenye utawala wake katika ya 1978 na 2002.

Wadadisi wanasema kuwa migawanyiko hiyo ilianza mnamo 1976, baada ya kuibuka kwa kundi la ‘Change the Constitution Movement’ lililopinga mpango wa Bw Moi kumrithi Mzee Jomo Kenyatta baada ya kifo chake mnamo 1978.

Kundi hilo liliwashirikisha wanasiasa kama Kihika Kimani, Njenga Karume, Dkt Munyua Waiyaki kati ya wengine.

Wanasiasa hao walikuwa wameapa kufanya kila wawezalo kuhakikisha kuwa Bw Moi hakumrithi Mzee Kenyatta, kwa kushinikiza mageuzi ya katiba kumfungia Makamu wa Rais nje.

Hata hivyo, kuliibuka kambi nyingine tofauti iliyolipinga kundi hilo, iliyoapa kumtetea Bw Moi kwa kila hali.

Kundi hilo liliwashirikisha aliyekuwa Mwanasheria Mkuu Bw Charles Njonjo, mwanasiasa Godfrey Gitahi Kariuki (maarufu kama ‘GG’) na Rais Mstaafu Mwai Kibaki.

Kulingana na Prof Ngugi Njoroge, ambaye ni mwanahistoria na mchanganuzi wa siasa, uhasama wa makundi hayo mawili ulienea pakubwa na kuligawanya eneo la Mlima Kenya katika maeneo mawili; yaliyompinga na yaliyomuunga mkono Mzee Moi.

“Mzee Moi alitumia mgawanyiko wa makundi hayo mawili kupenya Mlimani, ambapo aliapa kumkabili yeyote ambaye angepinga shughuli za kuipigia debe Kanu,” akasema.

Wachanganuzi wanasema kuwa Bw Moi alitumia ushawishi wake kuwajenga wanasiasa walioendeleza ajenda zake katika sehemu mbalimbali za eneo hilo na kuwakabili wale ambao walijaribu kumkosoa.

Baadhi ya wanasiasa ambao aliwajenga ni aliyekuwa Waziri wa Elimu kwa muda mrefu Bw Joseph Kamotho (Murang’a), Mwangi Githiomi (Nyandarua), David Ngibu-ini (Nyeri), Jackson Angaine (Meru) kati ya wengine.

Prof Njoroge anasema kuwa Bw Moi aliwajenga wanasiasa hao kuwakabili wale ambao walionekana kupinga utawala wake katika maeneo hayo, ambapo wengi wao walikamatwa na kuwekwa kizuizini.

“Kundi hilo lilikuwa kama macho ya Bw Moi katika eneo la Mlima Kenya. Wale walioendesha harakati za kuipinga Kanu walifanya hivyo kwa kujihadhari sana ili kutogunduliwa na ‘majasusi wa kisiasa’ ambao Bw Moi alikuwa amewaweka ili kufuatilia shughuli zao. Wanasiasa hao walizua hofu na taharuki ya kisiasa, hali iliyoifanya Kanu kuogopwa sana,” asema mchanganuzi huyo.

Mbinu nyingine ambayo Mzee Moi alitumia ni kusambaratisha kilimo, ambacho ndicho kitegauchumi kikuu cha wenyeji wengi wa Mlima Kenya.

Wadadisi wanaeleza kuwa licha ya kukita kilimo kama mojawapo ya sekta kuu alizoimarisha sana ili kustawisha uchumi wa nchi, Mzee Moi alisambaratisha sekta hiyo kimakusudi kama “adhabu” kwa jamii za Agikuyu, Aembu na Ameru (GEMA) kuviunga mkono vyama vya kisiasa.

Vyama hivyo ni Ford-Asili kilichoongozwa na Bw Stanley Matiba, Democratic Party (DP) kilichoongozwa na Bw Kibaki kati ya vingine.

Vyama hivyo vilichipuka kama ishara ya uasi dhidi ya utawala wake.

“Mzee Moi aligundua kwamba uwezo wa kiuchumi wa jamii hizo ulitokana na ustawi wa sekta ya kilimo, ambapo ndipo zilionekana kutozimika kisiasa.

“Aliamua kuisambaratisha sekta hiyo kimakusudi, hasa baada ya uchaguzi mkuu wa 1992,” asema wakili Wahome Gikonyo, ambaye ni mchanganuzi wa siasa.

Ni wakati wa utawala wake ambapo bei ya kahawa, majanichai na pareto zilishuka sana, ambapo baadhi ya viwanda vilivyotumia kusagia mazao hayo pia vilifungwa katika hali tatanishi.

Mbinu nyingine ambayo Moi alidaiwa kutumia kulisambatatisha eneo hilo kisiasa ni kuwatia kizuizini wanasiasa ambao walikisiwa kuupinga utawala wake.

Wadadisi wanasema kuwa hiyo ndiyo sababu ambapo watu wengi ambao waliwekwa kizuizini katika utawala wa Moi wanatoka katika eneo hilo.

Baadhi ya wanasiasa na wanaharakati waliojipata pabaya ni Bw Matiba, Bw Charles Rubia, Koigi wa Wamwere, Wangari Mathai, Ngugi wa Thiong’o, Micere Githae Mugo, Maina wa Kinyatti, Wanyiri Kihoro kati ya wengine.Kulingana na Bw Gikonyo, nia ya Mzee Moi “kulinyamazisha” eneo la Mlima Kenya ndiyo iliwafanya wafungwa wengi wa kisiasa watoke humo.

“Wafungwa wengi wa kisiasa ambao waliteseka katika enzi ya Moi wanatoka katika jamii za Gema, kwani waligundua kwamba nia yake ilikuwa kuwanyamazisha kabisa, hasa baada ya jaribio la mapinduzi ya kijeshi mnamo 1982,” asema.

Wafungwa wengi wa kisiasa walilazimika kutorokea ughaibuni, kwani waliofia kwamba huenda wakadhulumiwa au hata kuuawa.

Kulingana na Bw Wamwere, kosa kuu ambalo eneo hilo lilifanya ni wanasiasa wake kutozungumza kwa sauti moja ili kumzuia Mzee Moi kuwatumia baadhi ya viongozi kuwasaliti na kuwanyamazisha wengine.

“Baadhi ya wale ambao walijipata kizuizini walisalitiwa na wenzao, baada ya “kununuliwa” na Mzee Moi, kwani aliwaahidi makuu,” asema Bw Wamwere, huku akisisitiza kuwa lazima eneo hilo lidumishe umoja wa kisiasa ili kuepuka mkosi kama huo.