Mbunge adai siasa humfanya kiongozi kuwa 'mbali' na Mungu
Na MARY WANGARI
KULINGANA na mbunge mmoja, ukubwa ni jaa.
“Ukitaka kuwa fukara haraka zaidi Kenya kuwa mbunge au diwani, na ukitaka kuwa mbali na Mungu na kuvutia laana kutoka kwa watu, kuwa mwanasiasa Kenya,” amesema Mbunge maalum wa Jubilee, David Ole Sankok.
Akizungumza Jumatano kupitia mahojiano ya simu, Sankok ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Kitaifa kuhusu Walemavu, amejutia uamuzi wake wa kujiunga na siasa akifichua kwamba amezorota kifedha tangu uteuzi wake bungeni mnamo 2017.
“Nilikuwa nimekaa raha mstarehe mno kabla ya kuwa mbunge. Sitawania muhula mwingine maadamu siasa za Kenya zinachosha mno ambapo kila mtu anafikiri una deni lao,” ameeleza.
Kulingana na naye, wanasiasa nchini hukabiliwa na kibarua kigumu ambapo raia huwajia na kila aina ya matatizo wakitarajia viongozi kuwasaidia.
“Siasa nchini Kenya ni ngumu mno. Ni mchezo mchafu ambapo kila mtu anafikiri wewe ni mali yake hasa mitandaoni. Kuna maafisa wengi mno wa umma lakini ni wanasiasa pekee wanaoandamwa kwa maombi ya michango hela za bure,” akasema.
Akaongeza: “Wabunge sawa na waajiriwa wengine hutegemea mishahara. Ni vigumu mno kupeana tu kiholela kitu ulichotolea jasho kama si jamaa au familia yako. Binafsi, sijazoea kupatiana vitu vya bure. Kama mlemavu, nimeng’ang’ana. Huwezi tu kupatiana hela bure pengine uwe umeiba. Ninawakilisha walemavu 6.5 milioni hata kama ningewapa kila mmoja Sh1 bado hazitoshi maadamu nina miradi mingeneyo inayonisubiri.”
Mbunge huyo mwenye umri wa miaka 41, alifichua kuwa sasa anajiandaa kustaafu mapema kutoka ulingo wa siasa huku akielekeza macho yake kwa Umoja wa Mataifa kama mshauri maalum kuhusu walemavu ambapo anahisi atachangia zaidi ikizingatiwa rekodi yake katika kipindi alichohudumu nchini.
Mwanasiasa huyo ambaye pia ni mfanyabiashara maarufu anayemiliki kliniki, hoteli Narok na pia yuko katika biashara ya ustawishaji, atakumbwa kwa mchango wake kuhusu sheria kadha kuhusu walemavu ikiwemo: ununuzi wa zabuni za serikali kwa walemavu, uanzilishi wa lugha ya ishara kama lugha ya tatu Kenya, mitihani faafu kwa walemavu na mfumo jumuishi wa elimu Kenya.