Mbunge Sabina Chege aunda mswada kulazimu maafisa kutumia hospitali za umma
BAADHI ya wabunge waliunga mkono hoja iliyowasilishwa bungeni na Mbunge Maalum Bi Sabina Chege, inayopendekeza kuwa maafisa wote wa umma wawe wakitibiwa katika vituo vya afya vya umma badala ya hospitali za kibinafsi.
Bi Chege alisema kuwa maafisa hao huendea matibabu katika hospitali za kibinafsi zinazotoza ada ya juu, ambapo gharama hizo hulipwa na serikali kupitia bima ya afya.
Alisisitiza kuwa mamilioni ya pesa zinazotolewa kwa hospitali za binafsi kupitia bima hizo zinaweza kuelekezwa kwenye hospitali za serikali ili kuboresha huduma na miundomsingi.
“Serikali haihitaji kuongeza pesa zaidi. Fedha hizo zinazolipwa kwa bima zikitumika vizuri, zitaboresha hospitali zetu, kuongeza idadi ya madaktari na kuhakikisha mazingira safi ya kutoa huduma,” alisema Bi Chege.
Aliibua masikitiko kuwa licha ya wananchi kulipia Bima ya Afya ya Jamii (SHA), wengi hulazimika kununua dawa nje ya hospitali kwa sababu ya ukosefu wa dawa na vifaa.
Aidha, alidai kuwa kuna watu wachache wanaofaidika kutokana na ulegevu wa huduma katika hospitali za umma kwa kuhakikisha vifaa havifanyi kazi, hali inayowalazimu wagonjwa kuhamia hospitali binafsi.
Bi Chege alipendekeza Kamati ya Afya ya Bunge kuchunguza matumizi ya fedha za SHA, akisema ni asilimia 42 pekee ya pesa hizo ndiyo huelekezwa kwa hospitali za umma, huku asilimia kubwa ikifaidi hospitali binafsi.
“Kwa nini Shilingi milioni 100 zilipwe kwa hospitali binafsi ndogo inayotoa huduma za saratani badala ya kuelekeza fedha hizo kwenye hospitali za rufaa za serikali?” Alihoji.
Mbunge wa Lamu Mashariki, Bi Ruweida Obo, alitaka serikali iweke sheria kali zitakazowazuia maafisa wa umma kutibiwa katika hospitali za binafsi. Alisema kuwa mfano wa viongozi ndio utakaowashawishi wananchi kuwa na imani na hospitali za serikali.
“Ikiwa sisi viongozi tutatumia hospitali za serikali, basi wananchi nao wataamini huduma hizo. Tuanzie na sisi wenyewe,” alisema.
Kwa upande wake, Mbunge wa Marakwet Mashariki, Bw David Kangongo Bowen, alisema hoja hiyo itapobadilishwa kuwa sheria, itawapa wananchi nafasi ya kupata huduma bora za afya. Alitaja huduma duni katika hospitali za serikali kuwa sababu kuu ya maafisa wengi wa umma kuzikwepa.
“Hebu angalia Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta ambayo ilijengwa kwa gharama kubwa. Hadi sasa, ni vigumu kwa afisa wa umma kupata matibabu pale, ilhali madaktari wanaofanya kazi hospitali binafsi pia huhudumu huko,” alisema.
Mbunge wa Lang’ata, Bw Felix Odiwour almaarufu Jalang’o, alipendekeza kuwa wale wanaotaka kutibiwa katika hospitali za binafsi watumie pesa zao binafsi na si fedha za umma.
“Sheria iwe wazi: kila mmoja atibiwe hospitali ya umma. Kwa wale wanaotaka kwenda hospitali binafsi, wasitumie pesa za ushuru wa mwananchi bali pesa zao wenyewe. Pia, kampuni za bima zifahamishwe kuwa hazifai kulipia huduma hizo kwa viongozi,” alisema.