Habari

Mbunge wa zamani Sammy Mwaita ashtakiwa kwa ulaghai wa ardhi

Na RICHARD MUNGUTI August 4th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

ALIYEKUWA Mbunge wa Baringo ya Kati Sammy Silas Komen Mwaita ameshtakiwa kwa ulaghai wa shamba la Sh300 milioni anaodaiwa alitekeleza miaka 24 iliyopita alipokuwa Kamishna wa Ardhi.

Bw Mwaita alikabiliwa na mashtaka sita ya, kula njama kulaghai shamba, ughushi wa hati miliki, utumizi mbaya wa mamlaka na kutoa habari za uwongo kwa afisa wa polisi.

Mbunge huyo wa zamani ameshtakiwa pamoja na mfanyabiashara Brian Kiptoo Kiplagat. Aliachiliwa kwa dhamana ya Sh10 milioni ama Sh2 milioni pesa tasilimu.

Wote wawili wameshtakiwa kula njama kuwalaghai Rose Njoki Kang’au na Mucugu Wagatharia mashamba yao katika eneo la Nairobi West.

Mwaita ameshtakiwa kutumia mamlaka yake vibaya kuandikisha mashamba ya Njoki na Mucugu kwa jina la kampuni ijulikanayo kwa jina Shaba Trustees Limited.

Mbunge wa zamani wa Baringo ya Kati Sammy Mwaita alipofikishwa kortini Agosti 4, 2025 kwa ulaghai wa ardhi wa Sh300 milioni. Picha|Richard Munguti

Bw Mwaita alishtakiwa kutekeleza uhalifu huo mnamo Machi 30, 2001.

Bw Kiplagat hakufika kortini kujibu mashtaka.

Hata hivyo, hakimu mwandamizi mahakama ya Milimani Nairobi Bw Benmark Ekhubi alitoa agizo afike kortini Agosti 5, 2025 kujibu kesi dhidi yake.

Wakili anayemwakilisha Kiptoo alimweleza hakimu kwamba “mteja wake hakujua ikiwa alitakiwa kufika kortini.”

“Naamuru samansi ya Kiptoo ikabidhiwe wakili wake ampelekee afike kortini Jumanne mnamo Agosti 5, 2025 kujibu mashtaka,” Bw Ekhubi aliamuru.

Bw Mwaita aliyekamatwa Jumapili na maafisa wa polisi kutoka idara ya uchunguzi wa jinai (DCI) alikana mashtaka sita na kuomba aachiliwe kwa dhamana.

Kamishna huyo wa zamani wa ardhi (CoL) alishtakiwa baada ya mahakama kukataa kuahirisha kesi hiyo hadi Oktoba 15, 2025.

Hakimu alifahamishwa Majaji Alexander Muteti na Charles Gitonga Mbogo walifutilia mbali maagizo ya kumzuia Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) Renson Ingonga kutomshtaki mwanasiasa huyo.

Sammy Mwaita akiwa kortini Agosti 4 akisikiliza kesi ambapo ameshtakiwa kwa ulaghai wa shamba la Sh300 milioni Nairobi. Picha|Richard Muguti

“Hii kesi inasikizwa na hakimu mwandamizi Robinson Ondieki ambaye yuko likizoni. Kabla ya kuanza mapumziko aliorodhesha kesi hii itajwe Oktoba 15 mwaka huu ndipo Mwaita na Kiptoo wajibu shtaka,” Bw Ekhubi alielezwa na mawakili wa mbunge huyo wa zamani.

Pia hakimu alifahamishwa Mahakama ya Rufaa ilisikiza kesi iliyoshtakiwa na Njoki na Mucugu kuhusu umiliki wa shamba hilo kisha ikaamuliwa shamba hilo nambari ya usajili 209/9968 IR85847 A na B na ikaamuliwa inamilikiwa na Shaba Trustees Limited.

Akiomba mahakama ifutilie mbali hiyo kesi dhidi ya Mwaita, hakimu alielezwa mahakama ya rufaa iliamua kesi hiyo ilipotatua suala la umiki.