Habari

MCAs wamkaba Sakaja tena, watilia shaka kiwango cha mapato ya Kaunti

Na NDUBI MOTURI September 12th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

MADIWANI wa Kaunti ya Nairobi wanamtaka Gavana Johnson Sakaja kutoa hadharani maelezo kuhusu mahala palipo na “servers” za Nairobi Pay, mfumo wa kieletroniki unaotumiwa na serikali ya kaunti hiyo kukusanya mamilioni ya mapato kila siku.

Kupitia Mwenyekiti wa Kamati ya ICT na diwani wa Wadi ya Hospital, Mark Ruyi, madiwani hao pia wanataka nakala za taarifa za benki zinazoonyesha mapato yaliyokusanywa miaka iliyopita.

Kwenye mkutano wa kamati hiyo uliofanyika katika jengo la City Hall, baadhi ya madiwani walipuuzilia mbali kiwango cha pesa kilichotajwa na serikali ya kaunti hiyo wakisema ni “feki” kwa sababu stakabadhi husika hazikutolewa.

Diwani wa Kayole Jeremiah Themendu aliitaka Serikali ya Kaunti kuhakikisha kuna uwazi katika ukusanyaji na matumizi ya mapato.

“Sava za mtambo huu zimewekwa wapi? Ni pesa ngapi hukusanywa mbali na kiasi ambacho walitangaza. Mbona hatuwezi kulipa mishahara ilhali serikali hukusanya mapato kila siku?” akauliza.

Hata hivyo, Waziri wa Ubunifu na Uchumi wa Kidijitali Mike Gumo, anayesimamia kitengo cha ICT, alisisitiza kuwa Idara yake haiwezi kufikia mfumo huo wa ukusanyaji mapato.

“Wajibu wetu ni kutoa usaidizi. Tunahakikisha kuwa pesa zinafika kwenye akaunti kwa kurekebisha hitilafu za kimitambo. Hatuwezi kujua kiwango cha pesa katika akaunti kwa sababu hatuna idhini hiyo,” Bw Gumo akasema.

Alieleza kuwa Afisa Mkuu wa Fedha Asha Abdi ndiye msimamizi wa kipekee wa akaunti za kaunti katika benki na ndiye anayeweza kutoa taarifa za benki zinazohitajika.

Diwani wa Wadi ya Mathare North, Oscar Lore aliongeza kuwa bila taarifa kuhusu pesa zilizoko ndani ya akaunti za benki ni vigumu kuthibitisha kiwango cha mapato kilichoripotiwa.

“Suala kuu ni namna tunavyoweza kuthibitisha kama kiasi kilichoripotiwa na kaunti ni sahihi. Tunaweza tu kufanya tukiwa na stakabadhi zinazoonyesha pesa zinazoingia katika akaunti za Kaunti. Lakini tunapouliza, waziri wa kaunti hutuzungusha tu,” akasema.

Bw Ruyi, aliyeongoza kikao hicho, alihimiza serikali ya kaunti kuwasilisha stakabadhi mbele ya bunge kuwezesha kufuatiliwa kwa pesa zinazokusanywa na zinazotumiwa.

Mvutano huo ulijiri wakati ambapo serikali ya kaunti ya Nairobi, kupitia Katibu wa Kaunti Godfrey Akumali, alipotangaza mishahara ya mwezi Agosti 2025 itacheleweshwa baada ya Hazina ya Kitaifa kucheleweshwa utoaji wa fedha za mgao wa bajeti.

Wafanyakazi walielezwa kuwa serikali ya kaunti inafahamu fika kwamba ulipaji wa mishahara kwa wakati ni muhimu zaidi kwa kwamba “kaunti inaipa suala hilo kipaumbele inapoishinikiza Hazina ya Kitaifa kutoa fedha hizo.”

Katika mwaka wa kifedha uliopita Kaunti ya Nairobi iliandikisha ukasanyaji wa mapato ya kima cha Sh13.7 bilioni japo haikutimiza kiasi lengwa cha Sh20 bilioni.

Hata hivyo, wakaguzi wa hesabu wanasema wamenyimwa nafasi ya kupata maelezo kamili na data katika mfumo wa ukusanyaji mapato hali inayoathiri juhudi zao za kuthibitisha kiasi kamili cha mapato hayo.

Barua kadhaa ambazo wamemwandikia Gavana Johnson Sakaja wakitaka maelezo kuhusu suala hilo hazijajibiwa.