Habari

Mchakato wa kupata saini za BBI wang’oa nanga

November 25th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na WANDERI KAMAU

BAADA ya Tume ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kuafiki mchakato wa kukusanya sahihi za kuunga mkono mchakato wa kufanya mageuzi ya Katiba, Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM Raila Odinga wamekuwa miongoni mwa Wakenya wa kwanza kutia saini katika hafla iliyoandaliwa Jumba la Mikutano ya Kimataifa la Kenyatta (KICC) jijini Nairobi, Jumatano.

Shughuli hiyo ilifaa kuanza wiki iliyopita, kakini iligonga mwamba.

Akihutubu wakati huo, Rais Kenyatta amewataka Wakenya wawe watu wa kuishi kwa upendo na amani.

“Kulikuwa na joto la kisiasa baada ya uchaguzi wa mwaka 2017 na ndiposa mimi na Raila Odinga tukaketi chini na kuuwazia mpango wa kuitathmini Katiba ili kuleta stakabadhi ambayo itatufaa sisi Wakenya,” amesema Rais Kenyatta.

Baadhi ya viongozi ambao sahihi zao zimeshanakiliwa ni Isaac Ruto (Chama Cha Mashinani), Gavana wa Mombasa Ali Hassan Joho, Gavana wa Kitui Charity Ngilu, Mwenyekiti wa Baraza la Magavana Wycliff Oparanya, kiongozi wa Ford Kenya Moses Wetangula, Gavana wa Machakos Alfred Mutua, Katibu Mkuu wa Cotu Francis Atwoli miongoni mwa wengine.

IEBC imeidhinisha mwongozo na utaratibu ambao utafuatwa na viongozi wanaounga mkono ripoti ya BBI kukusanya sahihi kutoka kwa Wakenya.

Kwenye barua kwa kamati maalum inayosimamia uendeshaji wa shughuli hiyo, mwenyekiti wa IEBC, Bw Wafula Chebukati alisema kuwa tume imeidhinisha mfumo wa ukusanyaji sahihi baada ya kuutathmini.

Taarifa yake ilikuwa jibu kwa barua ambayo kamati hiyo iliiandikia tume hiyo mnamo Jumatano iliyopita, ikiitaka Tume kutathmini na kupitisha mfumo huo.

“Tume imetathmini ombi lenu na kuidhinisha utaratibu uliopendekezwa kuhusu ukusanyaji saini,” akasema Bw Chebukati.

“Ili kuruhusu mchakato huo kuendelea, lazima maelezo yote ya wale wanaounga mkono yajazwe kwa utaratibu uliotolewa,” akaeleza.

Kulingana na utaratibu, anayeunga mkono mpango huo atatakikana kujaza jina lake, namba ya kitambulisho au paspoti, kaunti anakotoka, eneobunge lake, wadi, kituo cha kupigia kura, namba ya simu na barua pepe.

Baadaye, atatia saini kuthibitisha ukweli kuhusu maelezo aliyotoa.

Hapo Jumatatu, kamati hiyo, ambayo inaongozwa na aliyekuwa mbunge wa Dagoretti, Dennis Waweru na Junet Mohamed (Suna Mashariki), ilisema inalenga kukusanya saini 4 milioni ikiwa ni tatu zaidi ya milioni moja zinazohitajika.

Katika kikao na wanahabari, wawili hao walisema uzinduzi rasmi wa mpango huo ungefanyika leo Jumatano katika Jumba la KICC, Nairobi jinsi ambavyo imefanyika.

Bw Waweru alisema baada ya uzinduzi, shughuli hiyo itaendelea katika kaunti zote 47.

“Kwa sasa, tunawaomba Wakenya wote wenye nia njema na wanaotaka kuona maovu mbalimbali yanaotukumba yakifika kikomo kujiunga nasi,” akasema Bw Waweru kwa niaba ya kamati hiyo.

Bw Mohamed alisema kuwa Mswada wa Mageuzi ya Katiba 2020, ambao ulikuwa umechelewesha zoezi hilo sasa uko tayari.

Wakati huo huo, mabunge ya kaunti za Nandi na Kericho yameiandikia barua Mahakama ya Juu, yakiitaka kutoa maoni yake kuhusu swali la mageuzi ya Katiba kati ya masuala mengine kuhusu mchakato wa BBI.

Mabunge hayo mawili yanataka ushauri kuhusu majukumu ya viongozi wa kisiasa katika mchakato mzima wa kura ya maamuzi.