Habari

Meli iliyojaa wageni wa majuu yawasili na kuchangamsha utalii

Na KNA January 13th, 2026 Kusoma ni dakika: 2

BANDARI ya Mombasa inatarajia kupokea angalau meli kumi za watalii katika robo ya kwanza ya mwaka huu, hali itakayoinua sekta ya utalii nchini.

Meli ya pili ya usafirishaji wa watalii mwaka huu ilitia nanga Mombasa mnamo Jumatatu, ikiwa na watalii zaidi ya 639 na wafanyakazi zaidi ya 300 kutoka nchi mbalimbali.

Akipokea meli hiyo kwa jina Azamara Journey, Waziri wa Utalii, Bi Rebecca Miano, alisema ongezeko la usafiri wa meli za kimataifa nchini ni ishara tosha kwamba raia wa kigeni wana imani na sekta ya utalii ya Kenya.

Alisema serikali inalenga kuongeza idadi ya wageni wa kimataifa kutoka milioni 2.4 mwaka 2024 hadi milioni 5.5 kufikia kipindi cha 2027 hadi 2028, huku mapato ya utalii yakilengwa kuongezeka kutoka Sh452 bilioni hadi Sh1 trilioni.

“Rais amesaidia sekta ya utalii kupitia mikakati mbalimbali. Sera ya anga wazi pia imevutia zaidi ya mashirika ya ndege Mombasa na Nairobi,” alisema.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari za Kenya (KPA), Kapteni William Ruto, alithibitisha kuwa Azamara Journey itafanya safari nne nchini mwaka huu.

“Jambo muhimu zaidi ni kwamba itakaa hapa kwa usiku mmoja, ikiruhusu abiria 663 na wafanyakazi 338 kufurahia jiji letu,” alisema Bw Ruto.

Alifichua kuwa kufikia Machi/Aprili, Mombasa itakuwa imepokea meli 10 za watalii. Meli nyingine yenye abiria zaidi ya 1,000 inatarajiwa kuwasili Jumatano kwa ziara ya siku moja.

“Wiki hii pekee, Mombasa itashughulikia zaidi ya watalii 2,000 watakaotembelea vivutio mbalimbali nchini,” alisema, akiongeza kuwa mafanikio hayo yametokana na juhudi za mashirika katika sekta ya utalii kutangaza Kenya kwa nchi za kigeni.

Bw Mohamed Hersi, Mkurugenzi wa Operesheni katika kampuni ya Pollmans Tours and Safaris iliyopanga safari ya meli hiyo, alisema karibu watalii 300 walipanga kufanya ziara za jijini, 250 wakielekea Hifadhi ya Taifa ya Tsavo Mashariki, na wengine wakisafiri kwa ndege kuelekea Maasai Mara na Amboseli.

“Utalii wa meli una manufaa si kwa Mombasa tu bali pia kaunti nyingine kama vile Narok, Taita Taveta, na Kajiado. Sehemu kubwa ya nchi inafaidika na sekta hii, na tunatarajia kuona meli nyingi zaidi zikifika kwenye bandari yetu,” alisema Bw Hersi.

Kapteni Antonio Toledo wa meli ya Azamara Journey, alieleza matumaini ya safari nyingi zaidi katika siku za usoni.

Waziri wa Utalii, Utamaduni na Biashara katika Kaunti ya Mombasa, Bw Mohamed Osman Ali, alisema mageuzi yaliyofanywa na serikali katika sekta ya utalii yameleta mafanikio yaliyo wazi.