Mgogoro wazuka Jubilee Party mwaniaji akikataa kujiondoa kura Mbeere North
TOFAUTI zimezuka kati ya uongozi wa Jubilee na mwaniaji wake wa ubunge katika eneobunge la Mbeere Kaskazini kuhusu iwapo chama hicho kitakuwa na mwaniaji au la.
Mwaniaji wa Jubilee, Bw Jacob Ireri Mbao amemkashifu vikali Naibu Katibu Mratibu wa chama Pauline Njoroge kutokana na kauli yake kuwa Jubilee haina mwaniaji kwenye uchaguzi huo wa Novemba 27, 2025.
“Bi Njoroge hana mamlaka ya kusema kuwa Jubilee haina mwaniaji na niko Jubilee wala siendi popote. Nitawania kwa kutumia chama hiki,” akasema Bw Mbao.
Bi Njoroge alikuwa amesema Jubilee itamuunga mkono Newton Karish wa DP aliyesema ndiye mwaniaji wa mrengo wa upinzani.
“Jubilee haina mwaniaji wala haijatoa tiketi kwa mgombeaji yeyote,” akasema Bi Njoroge.
Bw Mbao asiye na uwezo wa kusikia alisema kuwa alizungumza na Kiongozi wa Jubilee, Uhuru Kenyatta na Katibu Mkuu Jeremiah Kioni ambao waliahidi kumuunga kwenye kura hiyo.
“Tangu wawili hao waniidhinishe, sijapata habari zinazokinzana na msimamo huo kutoka kwao,” akaongeza.
Kiti hicho kilisalia wazi baada ya Geoffrey Ruku kuteuliwa Waziri wa Utumishi wa Umma.
Wawaniaji wengine wa kiti hicho ni Leonard Muthende wa UDA na Duncan Mbui wa Chama cha Kazi (CCK).