Mgomo wa wahadhiri : wasiwasi watanda wanafunzi wakitishia kuandamana
WANAFUNZI wa vyuo vikuu vya umma wametishia kuandamana kupinga kusimamishwa kwa masomo kwa wiki tatu kutokana na mgomo wa wahadhiri na wafanyakazi wengine wanaodai makubaliano mapya ya mishahara na marupurupu.
Baadhi ya wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Nairobi waliandamana Jumatano, huku wakionya kuwa kukosekana kwa suluhu kunaweza kuzua maandamano zaidi katika vyuo vingine.
Rais wa Muungano wa Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Nairobi, Ahmed Rashid, alisema mgomo huo unavuruga mipango ya masomo na kuongeza shinikizo za kifedha na kihisia kwa wanafunzi.
Alisema familia zao zinatarajia wamalize masomo, huku wengine wakikumbwa na matatizo ya kifedha.
Ian Ochieng, mwanafunzi wa chuo hicho, alisema usumbufu huo umekuwa ukijirudia kwa miaka mitatu mfululizo na kutishia kuungana na wahadhiri kugoma iwapo serikali haitachukua hatua.
Remmy Osoti, mwanafunzi wa mwaka wa nne katika Chuo Kikuu cha Multimedia, alisema wanafunzi wanaendelea kulipa gharama za chakula na malazi hata masomo yanapositishwa. Pia wanatumia fedha zaidi kusafiri nyumbani na kurejea vyuoni mgomo unapoisha.
Waziri wa Elimu Julius Ogamba alisema mazungumzo kuhusu makubaliano ya 2025–2029 yamekwama baada ya vyama vya wafanyakazi kukataa Sh9.7 bilioni ilizotoa serikali.
Alisema matakwa ya vyama hivyo yanakadiriwa kugharimu Sh100 bilioni, kiasi ambacho serikali inasema haiwezi kumudu kwa sasa.
Ogamba alisema wizara inazungumza na Wizara ya Fedha kuongeza pesa hizo na akatoa wito kwa wanafunzi kuwa watulivu.
Mwenyekiti wa kamati ya manaibu chansela wa vyuo vikuu vya umma, Profesa Daniel Mugendi, alionya kuwa muda uliopotea wa baadhi ya kozi, hasa udaktari, unaweza kukosa kufidiwa kwa sababu masomo yake hufuatana bila mapumziko.
Aliitaka serikali na vyama vya wafanyakazi kufikia makubaliano haraka ili kurejesha masomo na kuepusha migomo kama hiyo siku zijazo.