HabariHabari za Kitaifa

Wakuu wa shule wataka wabunge, wakaguzi kuepuka shule wakati wa mitihani

Na SAMUEL OWINO October 23rd, 2026 Kusoma ni dakika: 2

WAKUU  wa shule za umma wameomba Bunge kusitisha mikutano na ukaguzi kuhusu matumizi ya fedha za shule hadi mitihani ya kitaifa itakapokamilika, wakisema ziara za mara kwa mara zinavuruga maandalizi.

Ombi hilo liliwasilishwa na Mbunge wa Emuhaya, Omboko Milemba, ambaye pia ni mwenyekiti wa chama cha walimu wa shule za upili, Kuppet.

Wakuu hao wanataka wabunge, maafisa wa Wizara ya Elimu na wakaguzi wa hesabu wasitembelee shule wakati huu wa mitihani, wakisema hatua hiyo inakiuka mwongozo wa wizara unaozuia watu wasiohusika na mitihani kuingia shuleni.

Mitihani ya kitaifa ilianza Oktoba 19, 2026.

Shule za umma kwa sasa zinakaguliwa na taasisi tatu, ambazo ni Wizara ya Elimu, Ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali na Bunge kupitia Kamati ya Uwekezaji wa Umma kuhusu Utawala na Elimu.

Wizara ya Elimu hukagua shule katika viwango vya kaunti, kanda na kitaifa, huku Ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ikifanya ukaguzi katika kanda na kitaifa. Kamati ya Bunge nayo huchunguza ripoti za ukaguzi zinazowasilishwa bungeni.

Wakati mwingine, Kamati ya Bunge kuhusu Elimu pia hutembelea shule inapochunguza masuala yanayohitaji uchunguzi zaidi.

Milemba alisema ukaguzi huo  umewapa presha  wakuu wa shule wakati  ambao wanapaswa kusimamia mitihani.

Alisema wakuu wa shule pia ni wasimamizi wa vituo vya mitihani, hivyo wanapaswa kuelekeza nguvu zao katika kuhakikisha mitihani inaendeshwa vizuri badala ya kutumia muda mwingi kujibu maswali ya wakaguzi.

“Kuna ukaguzi mwingi mno katika shule za umma. Wakuu wa shule wanatumia muda mwingi kushughulikia maafisa wa Wizara ya Elimu, Ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali na wabunge,” alisema.

Hata hivyo, Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetang’ula alisema shule haziwezi kutumia kipindi cha mitihani kama sababu ya kukwepa uwajibikaji.

“Ni wazi kwamba uwajibikaji kuhusu matumizi ya rasilimali za umma si jambo la hiari. Ni wajibu wa kikatiba na wa msingi. Ukikabidhiwa rasilimali za umma, lazima utoe hesabu,” alisema.

Mbunge wa Gilgil, Martha Wangari, alisema ingawa hoja ya wakuu wa shule kuhusu muda wa ukaguzi ina msingi, haipaswi kutumiwa kuficha matumizi mabaya ya fedha.

Alidai kuwa baadhi ya walimu wanaokaribia kustaafu wamekuwa wakitumia fedha za shule na kuacha taasisi hizo zikiwa na madeni makubwa.

Mwenyekiti wa kamati hiyo, Dick Maungu, ambaye ni Mbunge wa Luanda, alisema Bunge halifanyi ukaguzi wa moja kwa moja shuleni bali huchunguza ripoti zinazowasilishwa na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali.

Alisema kuchunguza matumizi ya fedha za umma ni wajibu wa kikatiba wa Bunge, na kwamba wananchi wana haki ya kujua jinsi fedha hizo zinavyotumika.

Mbunge wa Nyando, Jared Okelo, pia alisema Bunge lina jukumu la kuhakikisha fedha zinazotolewa kwa shule kupitia mgao wa serikali zinatumika ipasavyo.