Habari

Mhubiri aliyeenda ziara ya utakaso Uganda anaswa akirejea na nyoka kwenye mkoba

Na SHABAN MAKOKHA May 7th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

MHUBIRI aliyekuwa katika ziara ya utakaso wa kiroho nchini Uganda alikamatwa akiwa na nyoka alipokuwa akijaribu kurudi Kenya kupitia Malenya, huku kukiwa na malalamishi kwamba baadhi ya viongozi wa kidini wasio waaminifu wanatumia uchawi.

Mchungaji Fanish Ramsey Maloba, mwenye umri wa miaka 26, alikamatwa na polisi waliokuwa kwenye doria mpakani Busia akiwa na nyoka mkubwa mweusi mwenye madoa ya kahawia, hali iliyozua taharuki miongoni mwa wakazi.

Polisi walisema kuwa mhubiri huyo alidai kuwa alivuka kwenda Uganda kwa maombi na kufukuza mapepo, na kwamba nyoka huyo alitokea ghafla na akamkamata kumtumia katika kanisa lake la Apostle Ministries lililoko Matayos.

Kukamatwa kwake kunajiri baada ya tukio sawa na hilo kutokea mwezi Novemba mwaka jana, ambapo mwanamke mmoja alifariki katika kijiji cha Murende, eneobunge la Matayos, baada ya kung’atwa na nyoka wa mhubiri wakati wa ibada ya kufukuza mapepo.

Marehemu, Margaret Agutu, pamoja na majirani wengine, walikuwa wamekusanyika kushuhudia kile kilichodaiwa kuwa muujiza wakati wa ‘ibada’ iliyokuwa inaendeshwa na mhubiri ambaye inadaiwa alikuwa akifanya matambiko kwa kutumia vifaa vya kishirikina, kabla ya kung’atwa na nyoka wa mchungaji huyo kwenye kidole na kufariki dunia alipokuwa akipelekwa hospitalini.
Mchungaji huyo alitoroka eneo hilo na nyoka wake baada ya hali ya mwanamke huyo kuwa mbaya zaidi.

Katika tukio jingine, mhubiri mmoja huko Lumakanda, Kaunti ya Kakamega alishambuliwa na nyoka mwenye sumu kali wakati wa jaribio lililofeli la kufukuza pepo wabaya katika kijiji cha Bendera, kufuatia malalamishi uhusu uchawi na mapepo eneo hilo.

Kamanda wa Polisi wa Kaunti ya Busia, Ahmed Abdille, alisema mhubiri huyo alikamatwa katika eneo la mpakani Malenya akiwa na nyoka huyo ambaye alikabidhiwa maafisa wa Huduma ya Wanyamapori Kenya (KWS).

“Tunamzuilia mshukiwa kwa kosa la kuwa na nyoka hai bila kibali halali kutoka KWS na uchunguzi umeanzishwa kubaini nyoka huyo alikuwa akikusudiwa kufanya nini. Pia tunachunguza kama alikuwa akisafirisha kiumbe huyo kuingia nchini kwa lengo la kuuza,” alisema Bw Abdille.

Inadaiwa mhubiri huyo alikuwa kwenye harakati za kuvuka tena kuingia Kenya akiwa na nyoka huyo aliyekuwa akikusudiwa kwa shughuli ya utakaso wa kiroho.

Kulingana na polisi, Maloba ambaye ana kanisa katika kituo cha biashara cha Matayos, alidai kuwa Roho Mtakatifu alimuongoza kumkamata nyoka huyo kuvunja nguvu za uchawi.

“Kwa sasa anazuiliwa katika Kituo cha Polisi cha Mayenje akisubiri kufikishwa Mahakamani kwa mashtaka yanayohusiana na umiliki haramu na usafirishaji wa wanyamapori,” aliongeza Bw Abdille.

Baadhi ya viongozi wa dini hutumia nyoka kuwadanganya waumini wao waamini kuwa maisha yao yatabadilika na matamanio yao kutimizwa ikiwa wataamini katika maombi yanayofanywa kupitia nyoka huyo.

Msururu wa matukio haya ya ajabu umeibua mashaka miongoni mwa umma kuhusu uhalali wa baadhi ya ‘miujiza ya kiroho’, huku wakazi wengi sasa wakijiuliza iwapo wachungaji hao huwasafirisha nyoka mapema ili kuigiza matukio ya kufukuza mapepo.

Pia inadaiwa kwamba kabla ya wachungaji hao kufika vijijini, huwapeleka mawakala wao kupanda mizimu au uchawi katika boma wanazolenga, kisha mchungaji hujitokeza kuiondoa mbele ya umati.