HabariHabari za Kitaifa

Mibabe saba kupimana nguvu kuwania ugavana Nairobi

Na JUSTUS OCHIENG November 4th, 2026 Kusoma ni dakika: 2

KUTOKA kwa rubani, wafanyabiashara, wabunge hadi viongozi wa kidini, uchaguzi wa ugavana Nairobi mwaka wa 2027 unatarajiwa kuwa na ushindani mkali huku wanasiasa sita wakimezea mate  usukani wa kaunti hiyo yenye ushawishi mkubwa kisiasa na kiuchumi.

Gavana wa sasa Johnson Sakaja, Mbunge wa Kasarani Ronald Karauri na Mbunge wa Makadara George Aladwa wanawania tiketi ya chama cha ODM, huku Mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino, Mbunge wa Embakasi Kaskazini James Gakuya na aliyekuwa Mbunge wa Starehe Margaret Wanjiru wakitafuta tiketi za vyama tofauti.

Aliyekuwa Katibu katika Wizara Irungu Nyakera na mfanyabiashara Agnes Kagure, ambao awali walikuwa wameonyesha nia ya kuwania kiti hicho, wameonekana kujiondoa katika kinyang’anyiro hicho.

Mashindano hayo yalipamba moto Jumatatu baada ya Bw Sakaja kuhama chama tawala cha United Democratic Alliance (UDA) na kujiunga rasmi na ODM, akitangaza azma ya kuwania muhula wa pili kupitia chama hicho.

Hatua hiyo imezua maswali kuhusu hatma ya wagombeaji wengine wa ODM ambao tayari walikuwa wameonyesha nia ya kuwania ugavana.

Bw Sakaja alipokelewa katika makao makuu ya ODM, Chungwa House, na viongozi wa chama hicho. Alisema kujiunga kwake hakukuwa mbinu ya kisiasa bali kurejea katika chama alichokuwa akihusishwa nacho.

“Baba (Raila Odinga) ndiye aliyeniambia nijiunge na ODM,” alisema, akirejelea uhusiano wake na mwanzilishi wa chama hicho aliyefariki.

Alisema anataka muhula mwingine ili kuendeleza huduma kwa wananchi, akisisitiza kuwa uongozi unapaswa kupimwa kwa jinsi maisha yanavyobadilika badala ya ushindi wa uchaguzi pekee.

Hata hivyo, Mwenyekiti wa ODM Nairobi George Aladwa amesema hatakubali wageni kupewa tiketi bila kupitia mchujo wa kidemokrasia.

“Safari ya kuongoza Nairobi lazima iongozwe na matakwa ya wananchi, haki na misingi ya demokrasia. Nimejizatiti katika maono yetu ya pamoja. Sauti ya wananchi lazima isikike,” alisema.

Bw Karauri, rubani wa zamani wa Kenya Airways na aliyekuwa Afisa Mkuu Mtendaji wa SportPesa, anasema uzoefu wake katika biashara, usafiri wa anga na siasa za eneo bunge unampa uwezo wa kusimamia Nairobi.

Alisema alifanya kazi Kenya Airways kwa miaka 11, mitano akiwa nahodha wa ndege, na amejifunza umuhimu wa uwajibikaji na mipango.

Ameahidi kuboresha ukusanyaji wa mapato, usafi wa jiji, mabomba  ya maji na barabara bila kuongeza ushuru. Pia anataka kukagua majengo ili kubaini yale yasiyo salama na kuhakikisha hospitali za kaunti zina dawa za kutosha.

Bw Karauri amemkosoa Sakaja, akisema kuhamia ODM hakutafuta kumbukumbu ya changamoto za uongozi wake, zikiwemo mafuriko, taka na majengo kuporomoka.

Kwa upande wake, Bw Gakuya anatumia uungwaji mkono wa kiongozi wa DCP na aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua kuimarisha kampeni zake. Ameahidi kubadilisha jaa la Dandora, kuunda nafasi za ajira na kurejesha hadhi ya Nairobi.

Bw Owino amechagua kuwania kupitia Mwananchi Party huku akiendelea kushirikiana na vuguvugu la Linda Mwananchi linalomuunga mkono  Seneta Edwin Sifuna kuwania urais.

Sifuna tayari amemtaja Owino kama mgombeaji  anayempendelea katika ugavana wa Nairobi.

Naye Bi Wanjiru, ambaye amepata chama cha Kenya Moja Movement, amesema hatasalimisha azma yake ya ugavana katika mazungumzo ya miungano.

Mchambuzi wa siasa Geoffrey Mboya anasema ODM inakabiliwa na changamoto ya kuamua kati ya kumpa kipaumbele gavana aliye madarakani, uaminifu wa wanachama wa muda mrefu au mgombeaji anayeweza kushinda.

Anasema Sakaja atapimwa kutokana na rekodi ya muhula wake wa kwanza, Aladwa atalazimika kuthibitisha umaarufu wake nje ya chama, huku Karauri akionyesha kuwa uzoefu wa biashara unaweza kutumika kusimamia kaunti.

Owino naye atalazimika kuthibitisha kuwa umaarufu wake unaenea nje ya Embakasi Mashariki, huku Gakuya akihitaji kupanua uungwaji mkono wa Gachagua na Wanjiru kujenga mtandao imara katika jiji lote.