HabariSiasa

Miguna apinga vikali juhudi za kubadili katiba

April 30th, 2018 Kusoma ni dakika: 2

Na VALENTINE OBARA

MWANAHARAKATI wa upinzani, Dkt Miguna Miguna, amepinga juhudi za marekebisho ya katiba zinazoshinikizwa na Kiongozi wa Chama cha ODM, Bw Raila Odinga.

Kulingana na wakili huyo aliyefurushwa nchini na serikali, Bw Odinga amepoteza mwelekeo kwa kuanzisha mikakati mipya ya kisiasa ilhali mapambano aliyoanzisha baada ya Rais Uhuru Kenyatta kutangazwa mshindi kwenye Uchaguzi Mkuu uliopita hayajazaa matunda.

“Hatutakaa kitako na kutazama Raila Odinga akidunisha na kuvuruga mapambano mengine ya kukomboa Kenya kikamilifu. Alifanya hivyo miaka ya 1997, 2002 na sasa ni 2018,” akasema kwenye msururu wa taarifa alizochapisha kwenye mitandao ya kijamii.

Aliongeza: “Hatutahadaiwa na kura nyingine ya maamuzi isiyo na maana. Tulikuwa na kura ya maamuzi mwaka wa 2005. Wakenya walifanikiwa kivipi kutokana nayo? Hakuna! Tunachotaka ni haki ya uchaguzi na kijamii wala si kura nyingine ya maamuzi isiyo na maana itakayogharimu kiasi kikubwa cha pesa.”

Bw Odinga amependekeza mfumo wa utawala wa ugatuzi urekebishwe, huku viongozi wengine wakiwemo wa kidini wakipendekeza utawala katika serikali kuu pia ubadilishwe ili kuwe na Waziri Mkuu na manaibu.

Kulingana naye, njia hii itawezesha utekelezaji wa maazimio ya kutatua changamoto ambazo zimekuwa zikikumba taifa ikiwemo utendaji wa haki na uwepo wa uongozi bora unaofaidi wananchi.

Hata hivyo, marekebisho ya katiba yamepingwa vikali na Naibu Rais William Ruto, pamoja na wandani wake wa kisiasa wanaoona ni njama ya kufanya viongozi wa upinzani kuingia serikalini kupitia njia ya mkato.

Dkt Miguna alimkashifu Bw Odinga na kusema ushirikiano wake na Rais Kenyatta ni usaliti kwa mamilioni ya Wakenya waliomuunga mkono katika uchaguzi uliopita, wakiwemo wananchi waliouawa na polisi walipokuwa wakiandamana kupinga matokeo ya uchaguzi wa urais.

Alipuuzilia mbali msimamo wa kigogo huyo wa kisiasa kwamba hatua yake inanuia kupatanisha Wakenya akadai ushirikiano wa wawili hao unalenga tu kuwanufaisha kibinafsi.

“Kwa kusalimu amri wakati ambapo tulikuwa tushakizidi nguvu Chama cha Jubilee, Raila Odinga aliimarisha nguvu za viongozi wadhalimu, akadhoofisha na kugawanya wafuasi wake,” akasema.

Hata hivyo, Mkurugenzi wa Mawasiliano katika Chama cha ODM, Bw Philip Etale, alimkosoa na kusema hatua ya Bw Odinga ilizuia vita na umwagikaji wa damu nchini.

“Wakenya wanataka amani, si kelele,” akasema Bw Etale.

Ingawa Bw Ruto amekuwa akidai marekebisho ya katiba yatatatiza juhudi za maendeleo, wachanganuzi wa kisiasa wamehusisha suala hilo na siasa za 2022 ambapo naibu wa rais anapanga kumrithi Rais Kenyatta atakayekamilisha hatamu yake ya pili ya uongozi ambayo ni ya mwisho kikatiba.